5
Hivyo Sulemani alipomaliza kazi ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la Mungu.
Sanduku la Agano laletwa Hekaluni
(1 Wafalme 8:1-9)
Kisha Sulemani akawaita huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila, na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Sayuni, Mji wa Daudi. Nao wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa mfalme wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba.
Wazee wote wa Israeli walipofika, Walawi wakajitwika Sanduku la Agano, nao wakalipandisha Sanduku na Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani, waliokuwa Walawi, walivibeba vitu hivyo, naye Mfalme Sulemani na kusanyiko lote la Israeli waliokuwa wamemzunguka wakasimama mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu za kondoo na ng’ombe nyingi kiasi kwamba idadi yao haikuweza kuandikwa au kuhesabika.
Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu hadi mahali patakatifu ndani ya Hekalu, pale Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi. Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kufunika Sanduku na mipiko yake ya kubebea. Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilizojitokeza kutoka Sanduku, nazo zilionekana ukiwa mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo. 10 Ndani ya Sanduku hapakuwa na kitu kingine chochote isipokuwa vile vibao viwili ambavyo Musa aliviweka ndani yake huko Horebu, mahali Mwenyezi Mungu alipofanya agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
11 Basi makuhani wakaondoka hapo Mahali Patakatifu. Makuhani wote waliokuwa huko walikuwa wamejiweka wakfu, bila kujali migawanyo yao. 12 Walawi wote waliokuwa waimbaji, yaani Asafu, Hemani, Yeduthuni, wana wa ndugu zao, walisimama upande wa mashariki wa madhabahu, wakiwa wamevaa kitani safi huku wakipiga matoazi, vinubi na zeze. Walikuwa pamoja na makuhani mia moja na ishirini wakipiga tarumbeta. 13 Wapiga tarumbeta na waimbaji wakaungana katika sauti linganifu, ikawa kama vile ni sauti moja, wakimsifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Nao wakapaza sauti zao, pamoja na tarumbeta na matoazi na vyombo vingine vya uimbaji, wakamsifu Mwenyezi Mungu, wakisema:
“Yeye ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.”
Ndipo Hekalu la Mwenyezi Mungu likajazwa na wingu, 14 nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulijaza Hekalu la Mungu.