6
Kuweka Hekalu wakfu
(1 Wafalme 8:12-21)
Ndipo Sulemani akasema, “Mwenyezi Mungu alisema kwamba ataishi katika giza nene. Nimejenga Hekalu zuri kwa ajili yako, mahali pako pa kukaa milele.”
Kusanyiko lote la Israeli walipokuwa wamesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. Kisha akasema:
“Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mikono yake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema, ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo ili Jina langu lipate kuwamo humo, wala sikumchagua mtu yeyote kuwa kiongozi wa watu wangu Israeli. Lakini sasa nimeuchagua Yerusalemu ili Jina langu lipate kuwamo humo, na nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’
“Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni mwili wako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’
10 “Mwenyezi Mungu ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 11 Nimeliweka humo Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuna lile Agano la Mwenyezi Mungu alilofanya na watu wa Israeli.”
Maombi ya Sulemani ya kuweka wakfu
(1 Wafalme 8:22-53)
12 Kisha Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu machoni pa kusanyiko lote la Israeli, naye akanyoosha mikono yake. 13 Basi Sulemani alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano na kimo chake dhiraa tatu, naye akaliweka katikati ya ukumbi wa nje. Akapanda juu ya hilo jukwaa kisha akapiga magoti mbele ya kusanyiko lote la Israeli, akanyoosha mikono yake kuelekea mbinguni. 14 Akasema:
“Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote. 15 Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.
16 “Sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiwa waangalifu katika yote wanayoyafanya na kuenenda mbele zangu kwa kuzingatia sheria zangu kama ulivyofanya.’ 17 Sasa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie.
18 “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani na wanadamu? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! 19 Hata hivyo sikiliza dua la mtumishi wako na maombi yake ya kuhurumiwa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambalo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. 20 Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. 21 Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia ukiwa mbinguni, makao yako, na unaposikia, samehe.
22 “Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili, 23 basi, sikia ukiwa mbinguni, ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimwadhibu yule mwenye hatia kwa kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake.
24 “Watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, 25 basi usikie ukiwa mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.
26 “Mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, 27 basi usikie ukiwa mbinguni, usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.
28 “Njaa au tauni vikija katika nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia, 29 kila dua au ombi litakalotolewa na yeyote kati ya watu wako Israeli, akitambua taabu zake na uchungu wake, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili, 30 basi usikie ukiwa mbinguni, makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote), 31 ili wakuogope na kuenenda katika utiifu kwako wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
32 “Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako kuu na mkono wako wenye nguvu ulionyooshwa, atakapokuja kuomba kuelekea Hekalu hili, 33 basi na usikie ukiwa mbinguni, makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli, nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.
34 “Watu wako watakapoenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa Mwenyezi Mungu kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 35 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, ukawape haki yao.
36 “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi iliyo mbali au karibu 37 na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya utumwa na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa na tumetenda uovu’; 38 wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 39 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, makao yako, ukawape haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako.
40 “Sasa, Mungu wangu, macho yako na yafumbuke na masikio yako yasikie maombi yanayoombwa katika mahali hapa.
41 “Sasa inuka, Ee Bwana Mwenyezi Mungu,
na uje mahali pako pa kupumzikia,
wewe na Sanduku la nguvu zako.
Makuhani wako, Ee Bwana Mwenyezi Mungu,
na wavikwe wokovu,
watakatifu wako na wafurahi
katika wema wako.
42 Ee Bwana Mwenyezi Mungu, usimkatae
mpakwa mafuta wako.
Kumbuka upendo mkuu uliomwahidia
Daudi mtumishi wako.”