7
Hekalu lawekwa wakfu
(1 Wafalme 8:62-66)
Baada ya Sulemani kumaliza kuomba, moto ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukalijaza Hekalu. Makuhani hawakuweza kuingia ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu kwa sababu utukufu wa Mwenyezi Mungu ulilijaza. Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa Mwenyezi Mungu ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu, nyuso zao zikigusa chini, wakamwabudu na kumshukuru Mwenyezi Mungu, wakisema,
“Yeye ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.”
Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu. Naye Mfalme Sulemani akatoa dhabihu ya ng’ombe elfu ishirini na mbili pamoja na kondoo na mbuzi elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mungu. Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao, vivyo hivyo Walawi wakiwa na vyombo vya uimbaji vya Mwenyezi Mungu ambavyo Mfalme Daudi alikuwa ametengeneza kwa ajili ya kumsifu Mwenyezi Mungu, navyo vilitumika aliposhukuru, akisema, “Fadhili zake zadumu milele.” Mkabala na Walawi, makuhani walipiga tarumbeta zao, nao Waisraeli wote walikuwa wamesimama.
Sulemani akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba aliyokuwa ametengeneza haikutosha kuweka sadaka hizo zote za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na za mafuta.
Hivyo Sulemani akaiadhimisha sikukuu wakati ule kwa muda wa siku saba, na Waisraeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Katika siku ya nane walifanya kusanyiko, kwa sababu walikuwa wameadhimisha kuwekwa wakfu kwa madhabahu kwa muda wa siku saba, na sikukuu kwa muda wa siku nyingine saba. 10 Katika siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba Sulemani akawaaga watu waende nyumbani mwao, wakishangilia na kufurahi mioyoni mwao, kwa wema mwingi Mwenyezi Mungu aliomtendea Daudi na Sulemani na kwa ajili ya watu wake Israeli.
Mwenyezi Mungu amtokea Sulemani
(1 Wafalme 9:1-9)
11 Sulemani alipomaliza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme, naye akiwa amefanikiwa kutenda yale yote aliyokuwa nayo moyoni mwake kufanya katika Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika jumba lake mwenyewe la kifalme, 12 Mwenyezi Mungu akamtokea Sulemani usiku na kumwambia:
“Nimesikia maombi yako nami nimechagua mahali hapa kwa ajili yangu mwenyewe kuwa Hekalu kwa ajili ya dhabihu.
13 “Nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu, 14 ikiwa watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekeza na kuomba na kuutafuta uso wangu, na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao, na nitaiponya nchi yao. 15 Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yanayoombwa mahali hapa. 16 Kwa maana sasa nimechagua na kutakasa Hekalu hili ili Jina langu lipate kuwa humo milele. Macho yangu na moyo wangu vitakuwepo daima.
17 “Kwako wewe, ukienenda mbele zangu kama Daudi baba yako alivyoenenda, na kufanya yote ninayokuamuru, nawe ukizishika amri zangu na sheria zangu, 18 nitakiimarisha kiti chako cha ufalme kama nilivyoagana na Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe mtu wa kutawala Israeli.’
19 “Lakini mkigeuka na kuyaacha maagizo na amri nilizowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, 20 ndipo nitakapoing’oa Israeli kutoka nchi yangu niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Nitalifanya kitu cha kudharauliwa na kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote. 21 Ingawa Hekalu hili linavutia sana sasa, wote watakaolipita watashangaa na kusema, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’ 22 Watu watajibu, ‘Ni kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, aliyewatoa Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”