8
Shughuli nyingine za Sulemani
(1 Wafalme 9:10-28)
Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alilijenga Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba lake mwenyewe la kifalme, Sulemani akajenga tena vijiji vile ambavyo Hiramu alikuwa amempa, naye akawapa Waisraeli waishi humo. Kisha Sulemani akaenda Hamath-Soba na kuuteka. Pia akajenga mji wa Tadmori katika jangwa, na miji yote ya kuhifadhia vitu katika Hamathi. Akajenga tena Beth-Horoni ya Juu na Beth-Horoni ya Chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo. Sulemani pia akajenga Baalathi na miji yake yote ya kuhifadhia vitu, na miji kwa ajili ya magari yake ya vita na kwa ajili ya farasi wake, chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni na katika nchi yote aliyotawala.
Watu wote waliosalia kutoka kwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (haya mataifa hayakuwa Waisraeli), yaani wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwa wamewaangamiza: hawa Sulemani akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo. Lakini Sulemani hakuwafanya Waisraeli watumwa kwa ajili ya kazi yake; hao ndio walikuwa wapiganaji wake, majemadari wake, maafisa wake, majemadari wa magari yake ya vita, na wapanda farasi wake. 10 Pia walikuwa maafisa wakuu wa Mfalme Sulemani, maafisa wakaguzi mia mbili na hamsini waliosimamia watu.
11 Sulemani akampandisha mke wake binti Farao kutoka Mji wa Daudi na kumleta jumba la kifalme alilokuwa amemjengea, kwa kuwa alisema, “Mke wangu hataishi katika jumba la kifalme la Daudi mfalme wa Israeli, kwa sababu mahali ambapo Sanduku la Mwenyezi Mungu limefika ni patakatifu.”
12 Mfalme Sulemani akamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu ambayo alikuwa ameijenga mbele ya ukumbi, 13 kulingana na mahitaji ya kila siku kwa ajili ya sadaka zilizoamriwa na Musa kwa ajili ya Sabato, Mwezi Mwandamo na sikukuu nyingine tatu za mwaka: Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma na Sikukuu ya Vibanda. 14 Kwa kushika maagizo ya Daudi baba yake, aliweka migawanyo ya makuhani kwa ajili ya kazi zao, nao Walawi kuongoza kusifu na kusaidia makuhani kufuatana na mahitaji ya kila siku. Pia akaweka mabawabu katika migawanyo kwa ajili ya malango mbalimbali, kwa sababu hivi ndivyo Daudi mtu wa Mungu alivyokuwa ameagiza. 15 Nao hawakuziacha amri za mfalme alizoamuru makuhani au Walawi katika jambo lolote, ikiwa ni pamoja na zile za hazina.
16 Kazi yote ya Mfalme Sulemani ilifanyika kuanzia siku msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu ulipowekwa hadi kukamilika kwake. Kwa hiyo Hekalu la Mwenyezi Mungu likamalizika kujengwa.
17 Ndipo Sulemani akaenda Esion-Geberi na Elathi katika pwani ya Edomu. 18 Naye Hiramu alimpelekea meli zilizoongozwa na maafisa wake mwenyewe, watu waliokuwa na ujuzi wa baharini. Hawa watu pamoja na wale wa Sulemani wakasafiri kwa bahari hadi Ofiri, wakaleta kutoka huko talanta mia nne na hamsini za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Sulemani.