9
Malkia wa Sheba amtembelea Sulemani
(1 Wafalme 10:1-13)
1 Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Sulemani, akaja Yerusalemu kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika akiwa na msafara mkubwa sana, wenye ngamia waliobeba vikolezo, dhahabu nyingi, na vito vya thamani. Alikuja kwa Sulemani na kuzungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. 2 Sulemani alimjibu maswali yake yote, wala hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwake hata asiweze kumwelezea. 3 Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, 4 chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, alipatwa na mshangao mkubwa.
5 Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. 6 Lakini sikuamini mambo yaliyosemwa hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana kuliko ile taarifa niliyoisikia. 7 Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wanaosimama mbele yako daima na kusikia hekima yako! 8 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe, na akakuweka kwenye kiti chake cha ufalme utawale kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Kwa sababu ya upendo wa Mungu wako kwa Israeli na shauku yake ya kuwathibitisha milele, amekufanya wewe mfalme juu yao, ili kudumisha haki na uadilifu.”
9 Naye akampa mfalme talanta mia moja na ishirini*Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5. za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezo na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa vikolezo vizuri kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Sulemani.
10 (Watumishi wa Hiramu na wa Sulemani wakaleta dhahabu kutoka Ofiri, tena wakaleta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani. 11 Mfalme akatumia hiyo miti ya msandali kuwa ngazi kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa Yuda tangu siku ile.)
12 Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, zaidi ya vile alivyokuwa amemletea mfalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
Fahari ya Sulemani
(1 Wafalme 10:14-25)
13 Uzito wa dhahabu ambayo Sulemani alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta mia sita sitini na sita (666)†Talanta 666 za dhahabu ni sawa na tani 25., 14 mbali na mapato yaliyoletwa na wafanyabiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.
15 Mfalme Sulemani akatengeneza ngao kubwa mia mbili kwa dhahabu iliyofuliwa. Kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli mia sita‡Shekeli 600 za dhahabu ni sawa na kilo 3.5.. 16 Akatengeneza pia ngao ndogo mia tatu za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu§Mane tatu za dhahabu ni sawa na kilo 1.7. za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.
17 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi. 18 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na mahali pa kuwekea miguu vyote vya dhahabu. Kila upande wa kiti ulikuwa na mahali pa kuegemeza mkono, na simba aliyesimama kando kila upande. 19 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote. 20 Vikombe vyote vya Mfalme Sulemani vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Sulemani. 21 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara*au: za Tarshishi(taz. 1 Wafalme 10:22; 22:48; 2 Nyakati 20:36; Isaya 2:16; 60:9). baharini zilizoendeshwa na watu wa Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo.
22 Mfalme Sulemani alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia. 23 Wafalme wote wa dunia wakatafuta kukutana na Sulemani ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake. 24 Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja, alileta zawadi, vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezo, farasi na nyumbu.
25 Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne kwa ajili ya farasi na magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita, na wengine akawa nao huko Yerusalemu. 26 Sulemani akatawala juu ya wafalme wote kuanzia Mto†yaani Mto Frati. hadi kwenye nchi ya Wafilisti na kuendelea hadi mpaka wa Misri. 27 Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima. 28 Farasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka nchi nyingine zote.
Kifo cha Sulemani
(1 Wafalme 11:41-43)
29 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Sulemani, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Nathani, katika unabii wa Ahiya Mshiloni na katika maono ya Ido mwonaji kuhusu Yeroboamu mwana wa Nebati? 30 Sulemani alitawala Israeli yote miaka arobaini akiwa Yerusalemu. 31 Kisha Sulemani akalala na baba zake, naye akazikwa katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
*9:9 Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5.
†9:13 Talanta 666 za dhahabu ni sawa na tani 25.
‡9:15 Shekeli 600 za dhahabu ni sawa na kilo 3.5.
§9:16 Mane tatu za dhahabu ni sawa na kilo 1.7.
*9:21 au: za Tarshishi(taz. 1 Wafalme 10:22; 22:48; 2 Nyakati 20:36; Isaya 2:16; 60:9).
†9:26 yaani Mto Frati.