10
Waisraeli wamwasi Rehoboamu
(1 Wafalme 12:1-20)
Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wameenda huko kumfanya mfalme. Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Sulemani), akarudi kutoka Misri. Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu; yeye na Waisraeli wote wakamwendea Rehoboamu na kumwambia, “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”
Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.
Kisha Mfalme Rehoboamu akataka ushauri kwa wazee ambao walimtumikia Sulemani baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri niwajibu nini watu hawa?”
Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”
Lakini Rehoboamu akakataa ushauri aliopewa na wazee, na akataka ushauri kwa vijana wa rika lake waliokuwa wakimtumikia. Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu’?”
10 Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Watu hawa walikuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ Wewe waambie, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11 Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.’ ”
12 Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” 13 Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Alikataa ushauri aliopewa na wazee, 14 akafuata ushauri wa vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.” 15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Mungu ili kutimiza neno ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amenena na Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia kwa Ahiya Mshiloni.
16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme:
“Je, tuna fungu gani kwa Daudi?
Tuna urithi gani kwa mwana wa Yese?
Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli,
angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!”
Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao. 17 Lakini kwa habari ya Waisraeli walioishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.
18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoniramu*au Adoramu; Kiebrania ni Hadoramu. aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu akafanikiwa kuingia kwenye gari lake la vita, akatorokea Yerusalemu. 19 Hivyo, Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.

*10:18 au Adoramu; Kiebrania ni Hadoramu.