11
Utabiri wa Shemaya
(1 Wafalme 12:21-24)
1 Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na ya Benyamini, vijana wenye uwezo elfu mia moja na themanini, ili kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli, na kuurudisha ufalme kwa Rehoboamu.
2 Lakini neno hili la Mwenyezi Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu: 3 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani mfalme wa Yuda, na Waisraeli wote walio Yuda na Benyamini, 4 ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Mwenyezi Mungu na kurudi, wakaacha kwenda kupigana dhidi ya Yeroboamu.
Rehoboamu ajengea Yuda ngome
5 Rehoboamu akaishi Yerusalemu akajenga miji yenye ngome katika Yuda: 6 Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa, 7 Beth-Suri, Soko, Adulamu, 8 Gathi, Maresha, Zifu, 9 Adoraimu, Lakishi, Azeka, 10 Sora, Aiyaloni na Hebroni. Hii ilikuwa miji yenye ngome katika Yuda na Benyamini. 11 Akaimarisha ulinzi wake na kuweka majemadari ndani yake, pamoja na maghala ya vyakula, ya mafuta ya zeituni, na ya divai. 12 Akaweka ngao na mikuki katika miji na kuifanya iwe imara sana. Kwa hiyo Yuda na Benyamini zikawa zake.
13 Makuhani na Walawi kutoka sehemu zote za Israeli wakawa upande wake. 14 Pia Walawi wakaacha maeneo yao ya malisho na mali yao, wakaja Yuda na Yerusalemu kwa sababu Yeroboamu na wanawe walikuwa wamewakataa wasiwe makuhani wa Mwenyezi Mungu. 15 Naye akawa amechagua makuhani wake mwenyewe kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia sanamu za mbuzi na za ndama ambazo alikuwa ametengeneza. 16 Wale waliotoka katika kila kabila la Israeli ambao walielekeza mioyo yao kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, wakawafuata Walawi huko Yerusalemu kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu, Mungu wa baba zao. 17 Wakaimarisha ufalme wa Yuda na kumuunga mkono Rehoboamu mwana wa Sulemani miaka mitatu, wakienenda katika njia za Daudi na Sulemani katika wakati huu.
Jamaa ya Rehoboamu
18 Rehoboamu alimwoa Mahalati aliyekuwa binti Yeremothi mwana wa Daudi; mamaye alikuwa Abihaili binti Eliabu mwana wa Yese. 19 Mahalati alimzalia Rehoboamu wana: Yeushi, Shemaria na Zahamu. 20 Kisha akamwoa Maaka binti Absalomu, aliyemzalia Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi. 21 Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wengine na masuria wake. Kwa jumla alikuwa na wake kumi na wanane na masuria sitini, wana ishirini na wanane na binti sitini.
22 Rehoboamu akamweka Abiya mwana wa Maaka, kuwa mkuu wa wana wa mfalme miongoni mwa ndugu zake ili amfanye mfalme. 23 Akatenda kwa busara, akiwasambaza baadhi ya wanawe katika wilaya zote za Yuda na Benyamini, pamoja na miji yote yenye ngome. Akawapa mahitaji tele na kuwaoza wake wengi.