12
Shishaki ashambulia Yerusalemu
(1 Wafalme 14:25-28)
Baada ya ufalme wa Rehoboamu kuimarika naye akawa na nguvu, yeye na Waisraeli wote waliiacha Torati ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu. Akiwa na magari ya vita elfu moja mia mbili, wapanda farasi elfu sitini, na idadi isiyohesabika ya majeshi ya Walibia, Wasukii na Wakushi waliokuja pamoja naye kutoka Misri. Akateka miji ya Yuda yenye ngome, akaendelea hadi Yerusalemu.
Ndipo nabii Shemaya akaja kwa Rehoboamu na kwa viongozi wa Yuda waliokuwa wamekusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya hofu ya Shishaki naye akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Ninyi mmeniacha, kwa hiyo, mimi nami sasa ninawaacha mkononi mwa Shishaki.’ ”
Viongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “Mwenyezi Mungu ni mwenye haki.”
Mwenyezi Mungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili la Mwenyezi Mungu likamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza, bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kupitia kwa Shishaki. Hata hivyo, watamtumikia Shishaki ili wapate kujifunza tofauti kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa nchi nyingine.”
Shishaki mfalme wa Misri alipoishambulia Yerusalemu, alichukua hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza. 10 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. 11 Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu walinzi walienda pamoja naye wakiwa wamebeba hizo ngao na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.
12 Kwa sababu Rehoboamu alijinyenyekeza, hasira ya Mwenyezi Mungu ikageukia mbali naye, hakuangamizwa kabisa. Kukawa na hali nzuri katika Yuda.
13 Mfalme Rehoboamu akajiweka imara katika Yerusalemu na akaendelea kuwa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na saba, mji ambao Mwenyezi Mungu alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili aliweke Jina lake humo. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni. 14 Rehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafuta Mwenyezi Mungu.
15 Kwa habari ya matukio katika utawala wa Rehoboamu, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Shemaya na mwonaji Ido zinazohusiana na vizazi? Kulikuwa na vita vya mara kwa mara kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. 16 Rehoboamu akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.