13
Abiya mfalme wa Yuda
(1 Wafalme 15:1-8)
Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu, Abiya akawa mfalme wa Yuda, naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka, binti*au mjukuu wa Urieli wa Gibea.
Basi kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu. Abiya aliingia vitani na jeshi la watu elfu mia nne wenye uwezo wa kupigana, naye Yeroboamu akapanga jeshi dhidi ya Abiya akiwa na jeshi la watu elfu mia nane wenye uwezo.
Abiya akasimama juu ya Mlima Semaraimu, katika nchi ya vilima ya Efraimu, naye akasema, “Yeroboamu na Waisraeli wote, nisikilizeni! Hamfahamu kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi na wazao wake ufalme juu ya Israeli milele kwa agano la chumvi? Hata hivyo Yeroboamu mwana wa Nebati afisa wa Sulemani mwana wa Daudi, aliasi dhidi ya bwana wake. Baadhi ya watu wasiofaa kitu, wabaya kabisa walimkusanyikia na kumpinga Rehoboamu mwana wa Sulemani alipokuwa kijana mdogo asiyekuwa na uamuzi, asiye na nguvu za kuweza kupingana nao.
“Hata sasa unapanga kupingana na ufalme wa Mwenyezi Mungu ambao uko mikononi mwa wazao wa Daudi. Kweli ninyi ni jeshi kubwa nanyi mnazo ndama za dhahabu Yeroboamu alizozitengeneza kuwa miungu yenu. Lakini je, hamkuwafukuza makuhani wa Mwenyezi Mungu, wana wa Haruni na Walawi na kujifanyia makuhani wenu wenyewe kama yafanyavyo mataifa ya nchi nyingine? Yeyote anayekuja kujiweka wakfu akiwa na ndama dume na kondoo dume saba aweza kuwa kuhani wa kile ambacho ni miungu kwenu.
10 “Lakini kwetu sisi, Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wetu, wala hatujamwacha. Makuhani wanaomtumikia Mwenyezi Mungu ni wana wa Haruni, nao Walawi wakiwasaidia. 11 Kila asubuhi na jioni wao hutoa sadaka za kuteketezwa na kufukiza uvumba wa harufu nzuri kwa Mwenyezi Mungu. Wao huweka mikate juu ya meza takatifu, na kuwasha taa kwenye kinara cha dhahabu kila jioni. Sisi tunazishika kanuni za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Lakini ninyi mmemwacha Mungu. 12 Mungu yu pamoja nasi; yeye ndiye kiongozi wetu. Makuhani wake wakiwa na tarumbeta zao watapiga baragumu ya vita dhidi yenu. Watu wa Israeli, msipigane dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, kwa maana hamtashinda.”
13 Basi Yeroboamu alikuwa ametuma jeshi kuzunguka nyuma ya Yuda ili akiwa mbele ya Yuda, jeshi liwavizie kwa nyuma. 14 Basi Yuda wakageuka na kuona kwamba wanashambuliwa mbele na nyuma. Ndipo wakamlilia Mwenyezi Mungu. Makuhani wakapiga tarumbeta zao, 15 nao wanaume wa Yuda wakapiga ukelele wa vita. Walipopiga ukelele wa vita, Mungu akawafukuza Yeroboamu na Waisraeli wote mbele ya Mfalme Abiya na Yuda. 16 Waisraeli wakakimbia mbele ya Yuda, naye Mungu akawatia mikononi mwao. 17 Abiya na askari wake wakawachinja kwa machinjo makuu, hata wakawepo majeruhi elfu mia tano miongoni mwa watu wenye uwezo wa Israeli. 18 Waisraeli walitiishwa katika tukio lile, nao watu wa Yuda wakawa washindi kwa sababu walimtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
19 Abiya akamfuatia Yeroboamu na kuteka miji ya Betheli, Yeshana na Efroni kutoka kwake, pamoja na vijiji vya miji hiyo. 20 Yeroboamu hakupata nguvu tena wakati wa utawala wa Abiya. Naye Mwenyezi Mungu akampiga Yeroboamu akafa.
21 Lakini Abiya akapata nguvu. Alioa wanawake kumi na wanne na alikuwa na wana ishirini na wawili na binti kumi na sita.
22 Matukio mengine ya utawala wa Abiya, pamoja na mambo aliyofanya na aliyosema, yameandikwa katika kitabu cha maelezo cha nabii Ido.

*13:2 au mjukuu wa