14
Asa mfalme wa Yuda
1 Naye Abiya akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika siku zake, nchi ikawa na amani kwa miaka kumi.
2 Asa akatenda yaliyo mema na haki machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wake. 3 Akaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu pa kuabudia, akayavunja yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Maashera. 4 Akawaamuru Yuda kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, na kutii sheria zake na amri zake. 5 Akaondoa mahali pa juu pa kuabudia na madhabahu za kufukizia uvumba kwenye kila mji katika Yuda, nao ufalme ulikuwa na amani katika utawala wake. 6 Akajenga miji yenye ngome katika Yuda, wakati nchi ikiwa na amani. Hakuna mtu yeyote aliyepigana vita naye katika miaka hiyo, kwa kuwa Mwenyezi Mungu alimpa amani.
7 Mfalme akawaambia Yuda, “Tuijenge hii miji na tuizungushie kuta, pamoja na minara, malango na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tumemtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tulimtafuta naye ametupatia amani kila upande.” Hivyo wakajenga na wakafanikiwa.
8 Asa alikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu kutoka Yuda, wenye ngao kubwa na mikuki, na jeshi la watu elfu mia mbili na themanini kutoka Benyamini, wenye ngao ndogo na pinde. Watu hawa wote walikuwa wapiganaji hodari.
9 Zera Mkushi akatoka kupigana dhidi yao akiwa na jeshi la watu maelfu ya maelfu na magari ya vita mia tatu, nao wakaja Maresha. 10 Asa akatoka kumkabili, nao wakapanga vita katika Bonde la Sefatha karibu na Maresha.
11 Kisha Asa akamlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kusema, “Ee Mwenyezi Mungu, hakuna yeyote aliye kama wewe wa kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Mungu wetu, kwa kuwa tunakutumainia wewe, nasi kwa jina lako tumekuja dhidi ya jeshi hili kubwa. Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Mungu wetu, usiwaache wanadamu wakushinde wewe.”
12 Mwenyezi Mungu akawapiga Wakushi mbele ya Asa na Yuda. Wakushi wakakimbia, 13 naye Asa na jeshi lake wakawafuatia hadi Gerari. Idadi kubwa ya Wakushi ilianguka hata wasiweze kuinuka tena, wakapondapondwa mbele za Mwenyezi Mungu na majeshi yake. Watu wa Yuda wakachukua nyara nyingi sana; 14 wakaangamiza vijiji vyote vya Gerari, kwa kuwa kicho cha Mwenyezi Mungu kilikuwa kimewaangukia. Wakateka nyara vijiji hivi vyote, kwani kulikuwa na nyara nyingi huko. 15 Pia wakashambulia kambi za wachunga makundi ya wanyama wakachukua na kuyaswaga makundi ya kondoo, mbuzi na ngamia. Kisha wakarudi Yerusalemu.