15
Asa afanya matengenezo
1 Roho wa Mungu akamjia Azaria mwana wa Odedi. 2 Akatoka ili kumlaki Asa na kumwambia, “Nisikilizeni, Asa na Yuda wote na Benyamini. Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi mkiwa pamoja naye. Mkimtafuta, ataonekana kwenu, lakini mkimwacha, naye atawaacha. 3 Kwa muda mrefu Israeli walikuwa hawana Mungu wa kweli, walikuwa hawana kuhani wa kuwafundisha na wala hawakuwa na sheria. 4 Lakini katika taabu yao walimrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, na kumtafuta, naye akaonekana kwao. 5 Katika siku hizo hapakuwa na amani kwa yeyote aliyesafiri, kutoka wala kuingia, kwa kuwa wakazi wote wa nchi walikuwa katika machafuko makubwa. 6 Taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ukapigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu alikuwa anawahangaisha kwa taabu za kila aina. 7 Lakini ninyi, kuweni hodari wala msikate tamaa, kwa kuwa mtapata thawabu kwa kazi yenu.”
8 Asa aliposikia maneno haya na unabii wa Azaria mwana wa Odedi yule nabii, akajipa moyo. Akaziondoa sanamu zote zilizokuwa machukizo katika nchi yote ya Yuda na Benyamini, na kutoka miji aliyoiteka katika nchi ya vilima ya Efraimu. Akakarabati madhabahu ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa mbele ya ukumbi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu.
9 Kisha akakutanisha Yuda wote, Benyamini na watu kutoka Efraimu, watu wa Manase na Simeoni walioishi miongoni mwao, kwa maana idadi kubwa walikuwa wamemjia kutoka Israeli walipoona kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.
10 Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Asa. 11 Wakati huo wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu za ng’ombe mia saba, kondoo na mbuzi elfu saba kutoka nyara walizoteka. 12 Wakafanya agano kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote. 13 Wale wote ambao hawangemtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, wangelazimika kuuawa, akiwa mdogo au mkubwa, mwanaume au mwanamke. 14 Wakamwapia Mwenyezi Mungu kwa sauti kuu, kwa kelele, na kupiga tarumbeta na mabaragumu. 15 Yuda wote wakafurahia kile kiapo kwa sababu walikuwa wameapa kwa moyo wao wote. Wakamtafuta Mungu kwa bidii, naye akaonekana kwao. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawapa amani pande zote.
16 Mfalme Asa akamwondolea Maaka, bibi yake, wadhifa wake kama mama malkia kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo, akaivunjavunja na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni. 17 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia katika Israeli, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Mwenyezi Mungu kikamilifu maisha yake yote. 18 Akaleta ndani ya Hekalu la Mungu fedha na dhahabu na vile vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.
19 Hapakuwa na vita tena hadi mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa.