16
Miaka ya mwisho ya Mfalme Asa
(1 Wafalme 15:17-24)
1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa Asa, Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.
2 Ndipo Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka hazina ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na kutoka jumba lake la kifalme na kumpelekea Ben-Hadadi mfalme wa Aramu, aliyekuwa anatawala huko Dameski. 3 Akasema, “Na pawe mkataba kati yangu na wewe, kama palivyokuwa kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee.”
4 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Wakashinda Iyoni, Dani, Abel-Maimu na miji yote ya hazina ya Naftali. 5 Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha kujenga Rama na kuacha kazi yake. 6 Ndipo Mfalme Asa akawaleta watu wote wa Yuda, nao wakachukua mawe na miti ambayo Baasha alikuwa anavitumia huko Rama. Kwa vitu hivyo akajenga Geba na Mispa.
7 Ikawa wakati huo mwonaji Hanani akamjia Mfalme Asa wa Yuda na kumwambia: “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Aramu nawe hukumtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wako, jeshi la mfalme wa Aramu limeponyoka mkononi mwako. 8 Je, hukumbuki lililotendeka kwa Wakushi na Walibia, hawakuwa jeshi lenye nguvu na magari mengi ya vita na wapanda farasi? Hata hivyo, ulipomtegemea Mwenyezi Mungu yeye aliwatia mkononi mwako. 9 Kwa kuwa macho ya Mwenyezi Mungu yanazunguka dunia yote ili kuwatia nguvu wale ambao mioyo yao inamtegemea kwa ukamilifu. Umefanya jambo la upumbavu, na kuanzia sasa na kuendelea utakuwa na vita.”
10 Asa akamkasirikia mwonaji kwa sababu ya jambo hili. Alikuwa ameghadhibika sana hata akamweka gerezani. Wakati huo huo Asa akaanza kuwatesa na kuwaonea baadhi ya watu kwa ukatili.
11 Matukio ya utawala wa Asa, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli. 12 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wake, Asa alishikwa na ugonjwa kwa miguu yake. Ingawa ugonjwa wake ulimzidia sana, hata katika kuugua kwake hakutafuta msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu bali kwa matabibu tu. 13 Katika mwaka wa arobaini na moja wa utawala wa Asa, alikufa, akalala na baba zake. 14 Nao wakamzika katika kaburi lile alilokuwa amejichongea katika Mji wa Daudi. Wakamzika kwa jeneza lililowekwa vikolezo na mchanganyiko wa manukato ya aina mbalimbali yaliyotengenezwa kwa utaalamu wa mtengeneza marashi, nao wakawasha moto mkubwa kwa heshima yake.