29
Hezekia mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 18:1-12)
1 Hezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria. 2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu kama Daudi baba yake alivyofanya.
3 Katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa utawala wake, alifungua milango ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, na kuikarabati. 4 Akawaingiza makuhani na Walawi ndani na kuwakutanisha katika uwanja upande wa mashariki 5 na kusema: “Nisikilizeni mimi, enyi Walawi! Jitakaseni nafsi zenu sasa, mkalitakase Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu. Ondoeni uchafu wote kutoka mahali patakatifu. 6 Baba zetu hawakuwa waaminifu, walifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na wakamwacha yeye. Wakageuza nyuso zao mbali na Maskani ya Mwenyezi Mungu wakamgeuzia visogo vyao. 7 Pia walifunga milango ya ukumbi wa Hekalu na kuzima taa zake. Hawakufukiza uvumba wala kutoa sadaka yoyote ya kuteketezwa katika mahali patakatifu kwa Mungu wa Israeli. 8 Kwa hiyo, hasira ya Mwenyezi Mungu ikashuka juu ya Yuda na Yerusalemu, naye akawa amewafanya kitu cha kutisha, cha kushangaza na kitu cha kufanyia mzaha kama mnavyoona kwa macho yenu wenyewe. 9 Hii ndiyo sababu baba zetu wameanguka kwa upanga na ndiyo sababu wana wetu wa kiume na wa kike, na pia wake zetu wamekuwa mateka. 10 Sasa ninadhamiria moyoni mwangu kufanya agano na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nasi. 11 Wanangu, basi msipuuze jambo hili sasa, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewachagua ninyi msimame mbele zake na kumtumikia, mkawe watumishi wake na mkamfukizie uvumba.”
12 Ndipo Walawi wafuatao wakaanza kazi:
Kutoka kwa Wakohathi,
Mahathi mwana wa Amasai na Yoeli mwana wa Azaria;
kutoka kwa Wamerari,
Kishi mwana wa Abdi na Azaria mwana wa Yahaleleli;
kutoka kwa Wagershoni,
Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;
13 kutoka kwa wana wa Elisafani,
Shimri na Yeieli;
kutoka kwa wana wa Asafu,
Zekaria na Matania;
14 kutoka kwa wana wa Hemani,
Yehieli na Shimei;
kutoka kwa wana wa Yeduthuni,
Shemaya na Uzieli.
15 Walipomaliza kuwakusanya ndugu zao na kujiweka wakfu, wakaingia ndani ili kutakasa Hekalu la Mwenyezi Mungu, kama vile mfalme alivyokuwa ameagiza, kwa kufuata neno la Mwenyezi Mungu. 16 Makuhani wakaingia patakatifu pa Hekalu la Mwenyezi Mungu ili kupatakasa. Wakatoa nje penye ua wa Hekalu la Mungu kila kitu kichafu walichokikuta kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu. Walawi wakavichukua na kuvipeleka nje katika Bonde la Kidroni. 17 Walianza kazi ya utakaso siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza na kufikia siku ya nane ya mwezi huo wakawa wamefikia kwenye ukumbi wa Mwenyezi Mungu. Kwa siku zingine nane wakalitakasa Hekalu la Mwenyezi Mungu lenyewe, wakakamilisha katika siku ya kumi na sita ya mwezi huo wa kwanza.
18 Kisha wakaingia ndani kwa Mfalme Hezekia kutoa habari na kusema: “Tumelitakasa Hekalu la Mwenyezi Mungu lote, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa pamoja na vyombo vyake vyote, meza ya kupanga mikate iliyowekwa wakfu, pamoja na vyombo vyake vyote. 19 Tumeviandaa na kuvitakasa vyombo vyote ambavyo Mfalme Ahazi, kwa kukosa uaminifu kwake, aliviondoa alipokuwa mfalme. Sasa viko mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu.”
Ibada Hekaluni yarejeshwa
20 Ndipo Mfalme Hezekia akainuka asubuhi na mapema, akakusanya maafisa wa mji wakakwea hekaluni mwa Mwenyezi Mungu. 21 Wakaleta mafahali saba, kondoo dume saba, wana-kondoo dume saba na beberu saba kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, kwa ajili ya mahali patakatifu na kwa ajili ya Yuda. Mfalme akawaamuru makuhani, wazao wa Haruni, kuvitoa vitu hivyo sadaka katika madhabahu ya Mwenyezi Mungu. 22 Hivyo wakachinja wale mafahali, nao makuhani wakachukua ile damu na kuinyunyiza kwenye madhabahu, halafu wakawachinja wale kondoo dume saba na kunyunyiza hiyo damu yao kwenye madhabahu, kisha wakawachinja wale wana-kondoo dume na kunyunyiza damu yao kwenye madhabahu. 23 Wale beberu waliokuwa kwa ajili ya sadaka ya dhambi wakaletwa mbele ya mfalme na kusanyiko nao wakaweka mikono yao juu hao beberu. 24 Ndipo makuhani wakawachinja hao beberu na kuweka damu yao kwenye madhabahu kwa ajili ya sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli wote, kwa sababu mfalme alikuwa ameamuru hiyo sadaka ya kuteketezwa na hiyo sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote.
25 Akawaweka Walawi kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu wakiwa na matoazi, vinubi na zeze kama ilivyoagizwa na Daudi na Gadi mwonaji wa mfalme pamoja na nabii Nathani kwani hili lilikuwa limeamriwa na Mwenyezi Mungu kupitia manabii wake. 26 Hivyo Walawi wakasimama tayari wakiwa na ala za uimbaji za Daudi na makuhani walikuwa na tarumbeta zao.
27 Hezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbia Mwenyezi Mungu pamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli. 28 Kusanyiko lote kusujudu katika kuabudu, huku waimbaji wakiimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea hadi walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.
29 Walipomaliza kutoa sadaka, mfalme na kila mtu aliyekuwa pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu. 30 Mfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifu Mwenyezi Mungu kwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha, nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.
31 Kisha Hezekia akasema, “Sasa mmejiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu. Njooni mlete dhabihu na sadaka za shukrani Hekaluni mwa Mwenyezi Mungu.” Hivyo kusanyiko likaleta dhabihu na sadaka za shukrani, nao wote waliokuwa na mioyo ya hiari wakaleta sadaka za kuteketezwa.
32 Idadi ya sadaka za kuteketezwa zilizoletwa na kusanyiko zilikuwa mafahali sabini, kondoo dume mia moja, na wana-kondoo dume mia mbili. Wote hawa walikuwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu. 33 Wanyama waliowekwa wakfu kwa sadaka ya kuteketezwa walikuwa mafahali mia sita, pamoja na kondoo na mbuzi elfu tatu. 34 Lakini makuhani walikuwa wachache sana kuweza kuchuna wale wanyama wote wa sadaka za kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia hadi kazi ile ikakamilika na hadi makuhani wengine walipowekwa wakfu, kwa kuwa Walawi walikuwa makini kujiweka wakfu kuliko makuhani. 35 Kulikuwa na sadaka nyingi za kuteketezwa, pamoja na mafuta ya wanyama ya sadaka za amani na sadaka za kinywaji ambazo ziliambatana na sadaka za kuteketezwa.
Kwa hiyo huduma ya Hekalu la Mwenyezi Mungu ikarudishwa kwa upya. 36 Hezekia pamoja na watu wote wakafurahi kwa sababu ya lile Mungu alilolifanya kwa ajili ya watu wake, kwa kuwa lilitendeka papo hapo.