30
Hezekia aadhimisha Pasaka
Hezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwa Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Mfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili. Kwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida. Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote. Wakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.
Kwa amri ya mfalme, matarishi wakazunguka Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake, zilizoandikwa:
“Watu wa Israeli, mrudieni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru. Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kutisha, kama mnavyoona. Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Mwenyezi Mungu. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi. Mkimrudia Mwenyezi Mungu, ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama mkimrudia yeye.”
10 Matarishi wakaenda mji hadi mji katika Efraimu na Manase, wakafika Zabuloni, lakini watu wakawadharau na kuwadhihaki. 11 Lakini, baadhi ya watu wa Asheri, Manase na Zabuloni, wakajinyenyekeza wakaja Yerusalemu. 12 Pia katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa juu ya watu kuwapa umoja katika kutenda yale ambayo mfalme na maafisa wake waliwaamuru, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu.
13 Basi umati mkubwa wa watu wakakusanyika huko Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu katika mwezi wa pili. 14 Wakajitia kazini kuyaondoa yale madhabahu yaliyokuwa huko Yerusalemu, wakayaondoa pia yale madhabahu ya kufukizia uvumba kwa miungu na kuyatupa Bonde la Kidroni.
15 Kisha wakamchinja mwana-kondoo wa Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketezwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. 16 Kisha wakachukua nafasi zao za kawaida kama ilivyoelezwa katika Torati ya Musa mtu wa Mungu. Makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa na Walawi. 17 Kwa kuwa wengi waliokuwa katika lile kusanyiko walikuwa hawajajitakasa, iliwapasa Walawi wachinje wana-kondoo wengine wa Pasaka kwa ajili ya wale watu ambao hawakuwa wametakaswa, ili kuwatakasa kwa Mwenyezi Mungu. 18 Ingawa watu wengi miongoni mwa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zabuloni walikuwa hawajajitakasa, hata hivyo walikula Pasaka kinyume na ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, “Mwenyezi Mungu, ambaye ni mwema na amsamehe kila mmoja 19 ambaye anauelekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zake, hata kama yeye si safi kulingana na sheria za mahali patakatifu.” 20 Naye Mwenyezi Mungu akamsikia Hezekia akawaponya watu.
21 Waisraeli waliokuwa Yerusalemu wakaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa muda wa siku saba, nao Walawi na makuhani walikuwa wakiimba kila siku, wakiwa na ala za uimbaji za kumsifu Mwenyezi Mungu.
22 Hezekia akazungumza akiwatia moyo Walawi wote, ambao walionesha ustadi katika kumtumikia Mwenyezi Mungu. Hivyo watu wakala chakula cha sikukuu kwa siku saba, wakitoa sadaka za amani na kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
23 Kisha kusanyiko lote wakakubali kuendelea na sikukuu kwa siku saba zaidi; kwa hiyo, kwa siku saba nyingine wakaendelea kuiadhimisha kwa furaha. 24 Hezekia, mfalme wa Yuda akatoa mafahali elfu moja, kondoo na mbuzi elfu saba kwa ajili ya kusanyiko, nao maafisa wakatoa mafahali elfu moja, pamoja na kondoo na mbuzi elfu kumi. Idadi kubwa ya makuhani wakajiweka wakfu. 25 Kusanyiko la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi, na wote waliokusanyika kutoka Israeli, pamoja na wageni waliotoka Israeli na wale walioishi Yuda, wote wakafurahi. 26 Kulikuwa na furaha kubwa katika Yerusalemu, kwa sababu tangu siku za Mfalme Sulemani mwana wa Daudi mfalme wa Israeli halijakuwepo jambo kama hili huko Yerusalemu. 27 Ndipo makuhani na Walawi wakasimama wakawabariki watu, naye Mungu akawasikia, kwa sababu maombi yao yalifika mbinguni, makao yake matakatifu.