33
Manase mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 21:1-18)
1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na tano. 2 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli. 3 Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia ambapo Hezekia baba yake, alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Mabaali na nguzo za Maashera. Akayasujudia majeshi yote ya angani na kuyaabudu. 4 Akajenga madhabahu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu ambamo Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litadumu Yerusalemu milele.” 5 Katika nyua zote mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. 6 Akawatoa kafara watoto wake kwa kuwapitishia motoni katika Bonde la Ben-Hinomu; akafanya ulozi, uaguzi, na uchawi, akatafuta ushauri kwa wenye pepo wa utambuzi na wenye kuwasiliana na mizimu. Akafanya maovu mengi machoni pa Mwenyezi Mungu, akaichochea hasira yake.
7 Akachukua ile sanamu aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu la Mungu ambalo Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Sulemani, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu, mji niliouchagua kutoka makabila yote ya Israeli, nitaliweka Jina langu milele. 8 Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli iondoke tena katika nchi niliyowapa baba zenu, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru kuhusu sheria zote, maagizo na amri zilizotolewa kwa mkono wa Musa.” 9 Lakini Manase akawaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu katika upotovu, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliangamiza mbele ya Waisraeli.
10 Mwenyezi Mungu akasema na Manase pamoja na watu wake, lakini hawakumjali. 11 Hivyo Mwenyezi Mungu akaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli. 12 Katika dhiki yake akamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake. 13 Naye alipomwomba, Mwenyezi Mungu akaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza dua lake. Kwa hiyo akamrudisha Yerusalemu na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu.
14 Baadaye akajenga ukuta wa nje wa Mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli; pia akaufanya mrefu zaidi. Akawaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome.
15 Akaondolea mbali miungu ya kigeni pamoja na sanamu kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Pia akaondoa madhabahu zote alizojenga katika kilima kilichojengwa Hekalu, na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji. 16 Kisha akarudisha madhabahu ya Mwenyezi Mungu na kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikie Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 17 Hata hivyo watu wakaendelea kutoa dhabihu mahali pa juu pa kuabudia, lakini wakawa wakimtolea Mwenyezi Mungu, Mungu wao, peke yake.
18 Matukio mengine ya utawala wa Manase, maombi yake kwa Mungu wake na maneno aliyoambiwa na waonaji walionena naye kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. 19 Maombi yake, pamoja na jinsi Mungu alivyoguswa na kusihi kwake, pia dhambi zake zote na kukosa uaminifu kwake, pamoja na sehemu alizojenga mahali pa juu pa kuabudia, na kusimamisha nguzo za Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekeza kwake: haya yote yameandikwa katika kumbukumbu za waonaji. 20 Manase akalala na baba zake, akazikwa katika jumba lake la kifalme. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
Amoni mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 21:19-26)
21 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. 22 Akatenda maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba yake Manase alivyofanya. Amoni akaabudu na kutoa dhabihu kwa sanamu zote alizokuwa ametengeneza Manase. 23 Lakini tofauti na Manase baba yake, hakujinyenyekeza mbele za Mwenyezi Mungu, badala yake Amoni alijiongeza hatia zaidi.
24 Watumishi wa Amoni wakampangia njama, nao wakamuua ndani ya jumba lake la kifalme. 25 Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamepanga njama dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.