34
Yosia afanya matengenezo
(2 Wafalme 22:1-2)
Yosia alikuwa na umri wa miaka nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na moja. Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia za Daudi baba yake, hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
Katika mwaka wa nane wa utawala wake, alipokuwa angali bado mdogo, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi baba yake. Katika mwaka wake wa kumi na mbili alianza kutakasa mahali pa juu pa kuabudia pa Yuda na Yerusalemu, akiondoa nguzo za Ashera, sanamu za kuchonga, na sanamu za kusubu. Mbele ya macho yake, wakazibomoa madhabahu za Mabaali, wakazivunja madhabahu za kufukizia uvumba zilizokuwa zimesimama juu yake, wakazivunja nguzo za Ashera, sanamu na vinyago. Hivi alivivunja vipande vipande na kutawanya juu ya makaburi ya waliokuwa wamevitolea sadaka. Akachoma mifupa ya makuhani wao juu ya madhabahu zao na kwa njia hiyo akaitakasa Yuda na Yerusalemu. Katika miji ya Manase, Efraimu na Simeoni, hadi Naftali na kwenye magofu yanayoizunguka, akavunja madhabahu na nguzo za Ashera na kuzipondaponda hizo sanamu hadi zikawa unga na kukata vipande vipande madhabahu zote za kufukizia uvumba katika nchi ya Israeli yote. Kisha akarudi Yerusalemu.
Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yosia, ili kutakasa nchi na Hekalu, akawatuma Shafani, mwana wa Azalia na Maaseya mtawala wa mji, pamoja na Yoa mwana wa Yoahazi, mwandishi ili kukarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
Wakamwendea Hilkia kuhani mkuu na kumpa fedha ambazo zilikuwa zimeletwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu ambazo Walawi waliokuwa mabawabu walikuwa wamezikusanya kutoka kwa watu wa Manase, Efraimu na mabaki wote wa Israeli kutoka kwa watu wote wa Yuda na Benyamini na wakazi wa Yerusalemu. 10 Kisha wakazikabidhi hizo fedha kwa watu waliowekwa ili kusimamia kazi ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hawa watu waliwalipa wafanyakazi waliokarabati na kutengeneza Hekalu lipate kurudi katika hali yake. 11 Wakawapa pia mafundi seremala na waashi fedha ili kununua mawe yaliyochongwa, mbao kwa ajili ya kufungia na boriti kwa ajili ya majengo ambayo wafalme wa Yuda walikuwa wameyaacha yakawa magofu.
12 Watu wakafanya kazi kwa uaminifu. Waliokuwa wamewekwa juu yao ili kuwaelekeza ni Yahathi na Obadia, Walawi wa uzao wa Merari, Zekaria na Meshulamu, waliotoka kwenye uzao wa Kohathi. Walawi wote wenye ujuzi wa kupiga ala za uimbaji, 13 wakawa wasimamizi wa vibarua na kuwaongoza wale waliofanya kila aina ya kazi. Baadhi ya Walawi walikuwa waandishi, maafisa na mabawabu.
Kitabu cha Torati chapatikana
(2 Wafalme 22:3-20)
14 Wakati walikuwa wakizitoa nje fedha zilizokuwa zimetolewa kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu, kuhani Hilkia akakipata kile Kitabu cha Torati ya Mwenyezi Mungu kilichokuwa kimetolewa kwa mkono wa Musa. 15 Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Torati ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” Akampa Shafani kile Kitabu.
16 Kisha Shafani akakipeleka kile Kitabu kwa mfalme na kumwambia, “Maafisa wako wanafanya kila kitu kama walivyokabidhiwa kufanya. 17 Wamelipa fedha zilizokuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu na wamewakabidhi wasimamizi na wafanyakazi.” 18 Kisha Shafani mwandishi akamwarifu mfalme kuwa, “Kuhani Hilkia amenipa Kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
19 Mfalme aliposikia yale maneno ya Torati, akayararua mavazi yake. 20 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, Shafani mwandishi na Asaya mtumishi wa mfalme, 21 “Nendeni mkamuulize Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu na kwa ajili ya mabaki waliosalia katika Israeli na Yuda, kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Mwenyezi Mungu iliyomwagwa juu yetu ni kubwa mno kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la Mwenyezi Mungu wala hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki.”
22 Hilkia pamoja na wale wote mfalme aliokuwa amewatuma pamoja naye wakaenda kuzungumza na nabii mke aitwaye Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tokhathi, mwana wa Hasra mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu, katika Mtaa wa Pili.
23 Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, 24 ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Nitaleta maafa mahali hapa na kwa watu wake: laana zote zilizoandikwa ndani ya kitabu hicho, ambazo zimesomwa mbele ya mfalme wa Yuda. 25 Kwa sababu wameniacha na kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kunighadhibisha kwa kazi yote ya mikono yao, hivyo hasira yangu itamwagwa mahali hapa, wala haitatulizwa.’ 26 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Mwenyezi Mungu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia: 27 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu na uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Mwenyezi Mungu. 28 Basi nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa na juu ya wote wanaoishi hapa.’ ”
Kwa hiyo wakampelekea mfalme jibu lake.
Yosia afanya agano la kutii
(2 Wafalme 23:1-20)
29 Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. 30 Akapanda kwenda hekaluni mwa Mwenyezi Mungu pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na Walawi, watu wote, wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, kilichokuwa kimepatikana katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. 31 Mfalme akasimama karibu na nguzo yake na kufanya upya agano mbele za Mwenyezi Mungu kwamba atamfuata Mwenyezi Mungu na kuzishika amri zake, maagizo na sheria zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, ili kuyatii maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
32 Ndipo akamtaka kila mmoja katika Yerusalemu na Benyamini kuweka ahadi zao wenyewe kwa hilo agano, watu wa Yerusalemu wakafanya hivyo kwa kufuata agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
33 Yosia akaondoa machukizo yote ya sanamu kutoka nchi yote ya Waisraeli na akawataka wale wote waliokuwa katika Israeli wamtumikie Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Kwa muda wote alioishi, hawakushindwa kumfuata Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.