10
Paulo atetea huduma yake
1 Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Al-Masihi, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! 2 Nawaomba nitakapokuja kwenu nisipaswe kuwa na ujasiri dhidi ya watu fulani kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata mtazamo wa ulimwengu huu. 3 Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4 Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. 5 Tunaangusha mawazo na kila kitu kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na kuteka nyara kila fikira ipate kumtii Al-Masihi. 6 Tena tunakuwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, hapo kutii kwenu kutakapokamilika.
7 Mnayaangalia yaliyo mbele ya macho yenu tu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Al-Masihi, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Al-Masihi, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo. 8 Basi hata nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana Isa alitupatia ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya. 9 Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu. 10 Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni mdhaifu, na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.” 11 Watu kama hao wajue ya kuwa yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi ndivyo tulivyo, na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.
12 Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonesha ya kuwa hawana busara. 13 Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ya huduma ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. 14 Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama ambavyo ingekuwa tusingekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Al-Masihi. 15 Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, ndivyo eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, 16 ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. 17 Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Mwenyezi Mungu.” 18 Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Mwenyezi Mungu humsifu.