11
Paulo na mitume wa uongo
1 Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo. 2 Ninawaonea wivu, wivu wa kiungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Al-Masihi kama mabikira safi. 3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Hawa alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Al-Masihi. 4 Kwa sababu mtu akija na kuwahubiria Isa mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.
5 Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu”. 6 Inawezekana mimi si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.
7 Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo? 8 Niliyanyang’anya makundi mengine ya waumini kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi. 9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nilipopungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walitimiza mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia. 10 Kwa hakika kama vile kweli ya Al-Masihi ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili. 11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda! 12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.
13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Al-Masihi. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.
Paulo ajivunia mateso yake
16 Nasema tena: mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. 17 Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi vile Bwana Isa angesema, bali kama mjinga. 18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. 19 Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! 20 Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida, au akiwanyang’anya, au akijitukuza mwenyewe, au akiwadanganya. 21 Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!
Lakini jambo lolote ambalo mtu mwingine angethubutu kujisifia, ninene kama mjinga, nami nathubutu kujisifu kuhusu hilo. 22 Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Ibrahimu? Mimi pia ni mzao wa Ibrahimu. 23 Je, wao ni watumishi wa Al-Masihi? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii zaidi yao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimepigwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. 24 Mara tano nimepigwa na Wayahudi mijeledi arobaini kasoro moja. 25 Mara tatu nilipigwa mijeledi, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nilivunjikiwa na meli, nilikaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa; 26 nimekuwa katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyang’anyi, hatari kutoka kwa Wayahudi wenzangu, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. 27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; nimejua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. 28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa kila siku na mzigo wa wajibu wangu kwa makundi yote ya waumini. 29 Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?
30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonesha udhaifu wangu. 31 Mungu na Baba*Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. wa Bwana wetu Isa, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. 32 Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata. 33 Lakini niliteremshwa kwa kapu kubwa kupitia dirisha ukutani, nikaokolewa kutoka mkononi mwake.