12
Maono ya Paulo na mwiba aliokuwa nao
1 Yanipasa nijisifu. Ingawa haifaidi kitu, nitanena kuhusu maono na mafunuo kutoka kwa Bwana Isa. 2 Namjua mtu mmoja katika Al-Masihi ambaye miaka kumi na nne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. 3 Nami najua kwamba mtu huyu, iwe ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, 4 alinyakuliwa hadi Paradiso*Paradiso maana yake bustani nzuri; hapa maana yake mbinguni.. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia. 5 Nitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu mwenyewe, ila nitajisifia udhaifu wangu. 6 Hata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema, 7 au kwa sababu ya mafunuo haya makuu. Ili kunizuia nisijivune, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili, nilimsihi Mwenyezi Mungu mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Al-Masihi ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu nafurahia katika udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida kwa ajili ya Al-Masihi. Kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.
Wasiwasi wa Paulo kwa Wakorintho
11 Nimejifanya mjinga, lakini mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ilinipasa kusifiwa na ninyi, kwa sababu mimi si dhalili kuliko wale “mitume walio bora”, ingawa mimi si kitu. 12 Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi. 13 Je, ninyi ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makundi mengine ya waumini, ila tu kwamba mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili!
14 Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara ya tatu. Nami sitawalemea, kwa sababu sihitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi. Kwa kuwa watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao. 15 Hivyo nitafurahi kutumia kila kitu nilicho nacho kwa ajili yenu, hata mwili wangu pia. Je, ninavyozidi kuwapenda, ndivyo upendo wenu kwangu unavyopungua? 16 Iwe iwavyo, kwa vyovyote vile, mimi sikuwalemea. Lakini wengine wanadhani mimi ni mjanja, nami niliwapata kwa hila! 17 Je, nilijipatia faida kwa kumtumia mtu yeyote niliyemtuma kwenu? 18 Nilimshawishi Tito aje kwenu, nami nilimtuma pamoja na ndugu yetu. Je, Tito aliwatumia ninyi ili kujipatia faida? Je, hatukuenenda kwa roho moja, na kwa hatua zile zile?
19 Je, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Al-Masihi. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu. 20 Kwa kuwa nina hofu kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko. 21 Nina hofu kwamba nitakapokuja tena kwenu, Mungu wangu atanidhili mbele yenu, nami nitasikitishwa na wengi waliotenda dhambi mbeleni, na wala hawajatubu kwa uchafu wao, uasherati, na ufisadi walioushiriki.