4
Mafuta ya mjane
Mke wa mmoja wa wana wa manabii akamlilia Al-Yasa, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu, amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha Mwenyezi Mungu. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.”
Al-Yasa akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?”
Akasema, “Mtumishi wako hana kitu chochote kabisa, isipokuwa mafuta kidogo.”
Al-Yasa akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache. Kisha ingia ndani na ujifungie mlango, wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, na kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.”
Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo, naye akaendelea kumimina mafuta. Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.”
Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka.
Yule mwanamke akaenda akamwambia yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”
Mwana wa Mshunami afufuliwa
Siku moja Al-Yasa akaenda Shunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo, naye akamsisitiza Al-Yasa aje kula chakula. Kwa hiyo kila mara alipitia pale, akaingia humo ili ale. Akamwambia mumewe, “Ninajua kwamba huyu mtu ambaye anakuja kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. 10 Tutengeneze chumba kidogo juu darini na tuweke ndani yake kitanda na meza, kiti na taa kwa ajili yake. Kisha anaweza kukaa humo kila mara akija kwetu.”
11 Siku moja Al-Yasa alipofika, akapanda chumbani kwake na kulala humo. 12 Akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyo Mshunami.” Hivyo akamwita, naye akaja akasimama mbele yake. 13 Al-Yasa akamwambia mtumishi wake, “Mwambie huyu mwanamke, ‘Umetaabika sana kwa ajili yetu. Sasa utendewe nini? Je, tunaweza kuzungumza na mfalme au jemadari wa jeshi kwa niaba yako?’ ”
Akajibu, “Mimi ninaishi kwangu miongoni mwa watu wangu.”
14 Al-Yasa akamuuliza mtumishi wake, “Je, ni nini kinachoweza kufanyika kwa ajili yake?”
Gehazi akasema, “Hakika, hana mwana, na mume wake ni mzee.”
15 Ndipo Al-Yasa akasema, “Mwite huyo mwanamke.” Kwa hiyo akamwita, naye akaja akasimama mlangoni. 16 Al-Yasa akamwambia, “Mwaka ujao, wakati kama huu utabeba mwana mikononi mwako.”
Yule mama akapinga, akasema, “La hasha, bwana wangu! Usimdanganye mtumishi wako, ee mtu wa Mungu!”
17 Lakini yule mwanamke akapata mimba, na mwaka uliofuata wakati kama ule ule akamzaa mwana, kama vile Al-Yasa alivyokuwa amemwambia.
18 Mtoto akakua, naye siku moja akamwendea baba yake, aliyekuwa pamoja na wavunaji. 19 Akamwambia baba yake, “Kichwa changu! Kichwa changu!”
Baba yake akamwambia mtumishi, “Mchukue umpeleke kwa mama yake.” 20 Baada ya mtumishi kumbeba na kumpeleka kwa mama yake, mtoto akaketi mapajani mwa mama yake hadi adhuhuri, kisha akafa. 21 Mama akampandisha na kumlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, kisha akafunga mlango, akatoka nje.
22 Akamwita mume wake na kusema, “Tafadhali mtume mmoja miongoni mwa mtumishi pamoja na punda ili niweze kwenda kwa mtu wa Mungu haraka na kurudi.”
23 Mume wake akamuuliza, “Kwa nini uende kwake leo? Leo si mwandamo wa mwezi, wala si Sabato.”
Mwanamke akasema, “Yote ni sawa.”
24 Akatandika punda na kumwambia mtumishi wake, “Mwongoze huyo punda. Usinipunguzie mwendo hadi nikuambie.” 25 Kwa hiyo akaenda na kumfikia huyo mtu wa Mungu katika Mlima Karmeli.
Alipomwona kwa mbali, huyo mtu wa Mungu akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Tazama, yule Mshunami! 26 Kimbia ukamlaki, umuulize, ‘Je, wewe hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto wako ni mzima?’ ”
Akasema, “Kila kitu ni sawasawa.”
27 Alipomfikia huyo mtu wa Mungu pale mlimani, akashika miguu yake. Gehazi akaja ili amwondoe, lakini yule mtu wa Mungu akasema, “Mwache! Yuko katika uchungu mkubwa, lakini Mwenyezi Mungu amenificha jambo hili na hajaniambia kwa nini.”
28 Yule mwanamke akasema, “Je, bwana wangu, mimi nilikuomba mwana? Je, sikukuambia, ‘Usiamshe matumaini yangu’?”
29 Al-Yasa akamwambia Gehazi, “Jikaze viuno, chukua fimbo yangu mkononi mwako na ukimbie. Ikiwa utakutana na mtu yeyote, usimsalimie, na mtu yeyote akikusalimu, usimjibu. Ilaze fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.”
30 Lakini mama mtoto akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo Al-Yasa akainuka, akafuatana naye.
31 Gehazi akatangulia mbele na kuilaza fimbo juu ya uso wa mtoto, lakini hapakuwa na sauti wala itikio. Hivyo Gehazi akarudi kukutana na Al-Yasa, na kumwambia, “Mtoto hajaamka.”
32 Al-Yasa alipofika kwenye ile nyumba, mtoto alikuwa amelala juu ya kitanda chake angali amekufa. 33 Akaingia ndani, akajifungia yeye na yule mtoto, akamwomba Mwenyezi Mungu. 34 Kisha akapanda kitandani, akalala juu ya yule mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, macho yake juu ya macho ya mtoto, mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Naye alipojinyoosha juu yake, mwili wa mtoto ukapata joto. 35 Al-Yasa akajiondoa juu yake na kuanza kutembeatembea ndani ya chumba, kisha akarudi tena kitandani na kujinyoosha tena juu ya mtoto mara nyingine. Mtoto akapiga chafya mara saba, akafungua macho yake.
36 Al-Yasa akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite huyo Mshunami.” Naye akafanya hivyo. Yule Mshunami alipokuja, Al-Yasa akasema, “Mchukue mwanao.” 37 Akaingia ndani, akaanguka miguuni pa Al-Yasa na kusujudu hadi chini. Kisha akamchukua mwanawe na kutoka nje.
Mauti ndani ya chungu
38 Al-Yasa akarudi Gilgali, nako huko kulikuwa na njaa katika eneo lile. Wana wa kundi la manabii walipokuwa wanakutana naye, akamwambia mtumishi wake, “Teleka chungu kikubwa jikoni uwapikie manabii.”
39 Mmoja wao akatoka kwenda mashambani kuchuma mboga na akapata mtango-mwitu. Akachuma matango na kujaza nguo yake aliyoikunja ili kubebea. Aliporudi, akayakatakata na kuyatumbukiza ndani ya chungu, ingawa hakuna aliyejua ni nini. 40 Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula.
41 Al-Yasa akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu chochote chenye madhara ndani ya chungu.
Watu mia wanalishwa
42 Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutoka kwa nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Al-Yasa akasema, “Wape watu ili wale.”
43 Mtumishi wake akamuuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia moja?”
Lakini Al-Yasa akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Watakula na kusaza.’ ” 44 Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu.