5
Naamani aponywa ukoma
Wakati huu, Naamani alikuwa jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu. Alikuwa mtu mkuu mbele ya bwana wake na aliyeheshimiwa sana, kwa sababu kupitia kwake, Mwenyezi Mungu alikuwa amewapa Aramu ushindi. Alikuwa askari hodari, lakini alikuwa na ukoma.*ukoma ni neno lililotumika kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi
Siku hizo vikosi kutoka Aramu vilikuwa vimeenda na vikawa vimemteka msichana kutoka Israeli, naye akamtumikia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, “Kama bwana wangu angemwona nabii aliye huko Samaria! Angemponya ukoma wake.”
Naamani akaenda kwa bwana wake na kumwambia alichosema yule msichana kutoka Israeli. Mfalme wa Aramuyaani Shamu akamjibu, “Hakika, nenda. Nitatuma barua kwa mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaondoka, akiwa amechukua talanta kumiTalanta 10 za fedha ni sawa na kilo 340. za fedha, shekeli elfu sita za dhahabu§Shekeli 6,000 za dhahabu ni sawa na kilo 70., na mavazi kumi. Barua aliyopelekea mfalme wa Israeli iliandikwa hivi: “Pamoja na barua hii ninamtuma mtumishi wangu, Naamani, kwako ili uweze kumponya ukoma wake.”
Mara mfalme wa Israeli alipomaliza kuisoma ile barua, akararua mavazi yake na kusema, “Je, mimi ni Mungu? Je, mimi naweza kuua na kufufua tena? Kwa nini huyu mtu anamtuma mtu ili mimi nipate kumponya ukoma wake? Tazama jinsi anavyotafuta kuanzisha ugomvi nami!”
Al-Yasa mtu wa Mungu aliposikia kwamba mfalme wa Israeli alikuwa amerarua mavazi yake, akamtumia ujumbe huu: “Kwa nini umerarua mavazi yako? Mwamuru mtu huyo aje kwangu, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaenda, akiwa na farasi wake na magari yake ya vita, na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Al-Yasa. 10 Al-Yasa akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.”
11 Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kupitisha mkono wake juu ya mahali penye ugonjwa ili aniponye ukoma wangu. 12 Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu.
13 Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, hungelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” 14 Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.
15 Kisha Naamani na wahudumu wake wote wakarudi kwa yule mtu wa Mungu. Akasimama mbele yake na kusema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu katika ulimwengu wote isipokuwa katika Israeli. Tafadhali sasa upokee zawadi kutoka kwa mtumishi wako.”
16 Nabii akajibu, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, ninayemtumikia, sitapokea kitu hata kimoja.” Ingawa Naamani alimsihi sana, yeye alikataa.
17 Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea, tafadhali mtumishi wako na apewe udongo kiasi cha mzigo wa kuweza kubebwa na punda wawili, kwa sababu mtumishi wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu. 18 Lakini Mwenyezi Mungu na amsamehe mtumishi wake kwa kitu hiki kimoja: Bwana wangu atakapoingia kwenye hekalu la Rimoni ili kusujudu, naye akiwa anauegemea mkono wangu, nami nikasujudu huko pia, wakati nitakaposujudu ndani ya hekalu la Rimoni, Mwenyezi Mungu na amsamehe mtumishi wako kwa ajili ya jambo hili.”
19 Al-Yasa akamwambia, “Nenda kwa amani.”
Baada ya Naamani kusafiri umbali fulani, 20 Gehazi, mtumishi wa Al-Yasa mtu wa Mungu, akajiambia mwenyewe, “Bwana wangu amemwachia kirahisi sana Naamani, huyu Mwaramu*au Mshami, kwa kutokupokea kutoka kwake vile alivyovileta. Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, nitamkimbilia na kupata kitu kutoka kwake.”
21 Hivyo Gehazi akaharakisha kumfuatilia Naamani. Naamani alipomwona akikimbia kumwelekea, akashuka chini kutoka gari lake la vita na kwenda kumlaki. Akauliza, “Je, mambo yote ni sawa?”
22 Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedhaTalanta ni sawa na kilo 34. na mavazi mawili.’ ”
23 Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mavazi mawili. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi. 24 Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka. 25 Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Al-Yasa bwana wake.
Al-Yasa akamuuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?”
Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakuenda popote.”
26 Lakini Al-Yasa akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka gari lake la vita ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ng’ombe, au watumishi wa kiume na wa kike? 27 Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Al-Yasa, mwenye ukoma, mweupe kama theluji.

*5:1 ukoma ni neno lililotumika kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi

5:5 yaani Shamu

5:5 Talanta 10 za fedha ni sawa na kilo 340.

§5:5 Shekeli 6,000 za dhahabu ni sawa na kilo 70.

*5:20 au Mshami

5:22 Talanta ni sawa na kilo 34.