6
Shoka laelea
Wana wa manabii wakamwambia Al-Yasa, “Tazama, mahali hapa tunapokutana nawe ni padogo sana kwetu. Twendeni Yordani, ambapo kila mmoja wetu anaweza kupata nguzo moja, nasi tujenge huko mahali petu pa kuishi.”
Naye akawaambia, “Nendeni.”
Kisha mmoja wao akasema, “Je, tafadhali, huwezi kufuatana na watumishi wako?”
Al-Yasa akajibu, “Nitakuja.” Naye akaenda pamoja nao.
Basi wakaenda Yordani, nao wakaanza kukata miti. Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akalia, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!”
Mtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonesha mahali penyewe, Al-Yasa akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea. Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyoosha mkono wake, akalichukua.
Al-Yasa awanasa Waaramu waliopofushwa
Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.”
Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.” 10 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Al-Yasa alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo.
11 Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?”
12 Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Al-Yasa, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.”
13 Mfalme akaagiza akisema, “Nendeni, mkatafute aliko, ili niweze kutuma watu kumkamata.” Taarifa ikarudi kwamba, “Yuko Dothani.” 14 Ndipo akatuma farasi na magari ya vita na jeshi lenye nguvu huko. Walienda usiku na kuuzunguka mji.
15 Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”
16 Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”
17 Kisha Al-Yasa akaomba, “Ee Mwenyezi Mungu, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Mwenyezi Mungu akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya vita yaliyowaka moto yamemzunguka Al-Yasa pande zote.
18 Adui waliposhuka kumwelekea, Al-Yasa akamwomba Mwenyezi Mungu: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Al-Yasa alivyoomba.
19 Al-Yasa akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria.
20 Baada ya kuingia mjini, Al-Yasa akasema, “Mwenyezi Mungu, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo Mwenyezi Mungu akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.
21 Wakati mfalme wa Israeli aliwaona, akamuuliza Al-Yasa, “Je, baba yangu, niwaue?”
22 Naye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.” 23 Basi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.
Njaa katika Samaria iliyozingirwa
24 Baada ya kitambo kidogo, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akaandaa jeshi lake lote akapanda kwenda kuizingira Samaria. 25 Kukawa na njaa kuu katika mji. Samaria ilizingirwa kwa muda mrefu, kiasi kwamba kichwa cha punda kiliuzwa kwa shekeli themanini*Shekeli 80 za fedha ni sawa na kilo moja. za fedha, na robo ya kibabaRobo ya kibaba ni sawa na lita 0.3. cha mavi ya njiwa kiliuzwa kwa shekeli tanoShekeli 5 ni sawa na gramu 55. za fedha.
26 Mfalme wa Israeli alipokuwa anapita juu ya ukuta, mwanamke mmoja akamlilia, “Bwana wangu mfalme, nisaidie!”
27 Mfalme akajibu, “Ikiwa Mwenyezi Mungu hakusaidii, nitakutolea wapi msaada? Je, ni kwenye sakafu ya kupuria? Au ni kwenye shinikizo la kukamulia zabibu?” 28 Kisha akamuuliza, “Kwani kuna nini?”
Yule mwanamke akamjibu, “Huyu mwanamke aliniambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla leo, na kesho tutamla mwanangu.’ 29 Basi tukampika mwanangu na kumla. Siku iliyofuata nikamwambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla.’ Lakini akawa amemficha.”
30 Mfalme aliposikia maneno ya yule mwanamke, akararua mavazi yake. Naye alipoendelea kutembea ukutani, watu wakamtazama, na ndani ya mavazi yake alikuwa amevaa gunia mwilini mwake. 31 Akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi ikiwa kichwa cha Al-Yasa mwana wa Shafati kitabaki juu ya mabega yake leo!”
32 Wakati huu, Al-Yasa alikuwa ameketi ndani ya nyumba yake, akiwa pamoja na wazee. Mfalme akatuma mjumbe kumtangulia, lakini kabla hajafika, Al-Yasa akawaambia wale wazee, “Hammwoni huyu muuaji jinsi anavyotuma mtu kukata kichwa changu? Tazama, wakati mjumbe huyo atakapofika, fungeni mlango na mzuieni asiingie. Je, vishindo vya nyayo za bwana wake haviko nyuma yake?”
33 Alipokuwa angali bado anazungumza nao, mjumbe akamfikia. Naye mfalme akasema, “Maafa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa nini niendelee kumngoja Mwenyezi Mungu zaidi?”

*6:25 Shekeli 80 za fedha ni sawa na kilo moja.

6:25 Robo ya kibaba ni sawa na lita 0.3.

6:25 Shekeli 5 ni sawa na gramu 55.