13
Yehoahazi mfalme wa Israeli
Katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wa Yoashi mwana wa Ahazia mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka kumi na saba. Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu kwa kufuata dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, na wala hakuziacha. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Israeli na kwa muda mrefu akawaweka chini ya utawala wa Hazaeli mfalme wa Aramu, na Ben-Hadadi mwanawe.
Ndipo Yehoahazi akamsihi Mwenyezi Mungu ampe rehema, naye Mwenyezi Mungu akamsikiliza, kwa maana aliona jinsi mfalme wa Aramu alivyokuwa akiwatesa Israeli vikali. Mwenyezi Mungu akamtoa mwokozi kwa ajili ya Israeli, nao wakaokoka kutoka mamlaka ya Aramu. Hivyo Waisraeli wakaishi katika nyumba zao wenyewe kama ilivyokuwa hapo awali. Lakini hawakuziacha dhambi za nyumba ya Yeroboamu, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, bali wakaendelea kuzitenda. Nguzo ya Ashera pia iliendelea kusimama katika Samaria.
Hapakubaki kitu chochote katika jeshi la Yehoahazi isipokuwa wapanda farasi hamsini, magari kumi ya vita na askari wa miguu elfu kumi, kwa kuwa mfalme wa Aramu alikuwa amewaangamiza hao wengine na kuwafanya kama mavumbi wakati wa kupura nafaka.
Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoahazi, yote aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Yehoahazi akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoashi*au Yoashi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Yehoashi mfalme wa Israeli
10 Katika mwaka wa thelathini na saba wa utawala wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala Israeli huko Samaria, naye akatawala miaka kumi na sita. 11 Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, na hakuacha dhambi yoyote kati ya zile za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, bali aliendelea kuzitenda.
12 Na kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, yote aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 13 Yehoashi akalala na baba zake, naye Yeroboamu akawa mfalme baada yake. Yehoashi akazikwa Samaria na wafalme wa Israeli.
14 Wakati huu, Al-Yasa alikuwa anaugua ugonjwa ambao baadaye ulimuua. Yehoashi mfalme wa Israeli akashuka kwenda kumwona na kumlilia. Akalia, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!”
15 Al-Yasa akasema, “Leta upinde na baadhi ya mishale,” naye mfalme akafanya hivyo. 16 Al-Yasa akamwambia mfalme wa Israeli, “Shika upinde mikononi mwako.” Alipokwisha kuuchukua, Al-Yasa akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
17 Al-Yasa akasema, “Fungua dirisha la mashariki,” naye akalifungua. Al-Yasa akasema, “Piga mshale!” Naye akapiga mshale. Al-Yasa akasema, “Mshale wa ushindi wa Mwenyezi Mungu, mshale wa ushindi juu ya Aramu! Utawaangamiza Waaramu kabisa huko Afeki.” 18 Kisha akasema, “Chukua mishale,” naye mfalme akaichukua. Al-Yasa akamwambia, “Piga ardhi kwa hiyo mishale.” Akaipiga mara tatu, halafu akaacha.
19 Mtu wa Mungu akamkasirikia na akasema, “Ungepiga chini mara tano au sita, ndipo ungeishinda Aramu na kuiangamiza kabisa. Lakini sasa utaishinda mara tatu tu.”
20 Al-Yasa akafa, nao wakamzika.
Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli. 21 Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Al-Yasa. Ile maiti ilipogusa mifupa ya Al-Yasa, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake.
22 Hazaeli mfalme wa Aramu aliwatesa Israeli wakati wote wa utawala wa Yehoahazi. 23 Lakini Mwenyezi Mungu akawarehemu na akawahurumia, akaonesha kujishughulisha nao kwa sababu ya agano lake na Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Hadi leo, hajawaangamiza wala kuwafukuza mbele zake.
24 Hazaeli mfalme wa Shamu akafa, naye Ben-Hadadi mwanawe akawa mfalme baada yake. 25 Kisha Yehoashi mwana wa Yehoahazi akateka tena kutoka kwa Ben-Hadadi mwana wa Hazaeli ile miji aliyokuwa ameitwaa kwa vita kutoka kwa baba yake Yehoahazi. Yehoashi alimshinda mara tatu, hivyo akaweza kuiteka tena ile miji ya Waisraeli.

*13:9 au Yoashi