14
Amazia mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 25)
1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu. 3 Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake.
4 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
5 Baada ya ufalme kuimarika mkononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake. 6 Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Musa, ambako Mwenyezi Mungu aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”
7 Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.
8 Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tukabiliane uso kwa uso.”
9 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. 10 Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani mwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
11 Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. 12 Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani mwake. 13 Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa mia nne*Dhiraa 400 ni sawa na mita 180.. 14 Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria.
15 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 16 Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa Samaria na wafalme wa Israeli. Naye Yeroboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
17 Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na tano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. 18 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amazia, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
19 Wakapanga njama dhidi ya Amazia huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuua huko. 20 Akarudishwa kwa farasi, akazikwa huko Yerusalemu pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi.
21 Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria†au Uzia aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, na kumfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake. 22 Ndiye aliijenga upya Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala na baba zake.
Yeroboamu wa pili mfalme wa Israeli
23 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, naye akatawala kwa miaka arobaini na moja. 24 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, na hakuacha dhambi hata moja ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda. 25 Ndiye alirudishia mipaka ya Israeli kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bahari ya Araba, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, lililosemwa kupitia mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii kutoka Gath-Heferi.
26 Mwenyezi Mungu alikuwa ameona jinsi kila mmoja katika Israeli, awe mtumwa au aliye huru, alivyoteseka kwa uchungu; hapakuwa na yeyote wa kuwasaidia. 27 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa hajasema kuwa atafuta jina la Israeli chini ya mbingu, akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.
28 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, yote aliyoyafanya na mafanikio yake ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyorudisha Dameski na Hamathi kwa Israeli, ambayo ilikuwa mali ya Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 29 Yeroboamu akalala na baba zake, wafalme wa Israeli. Naye Zekaria mwanawe akawa mfalme baada yake.