2 Timotheo
1
Salamu
1 Paulo mtume wa Al-Masihi Isa kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima ulio ndani ya Al-Masihi Isa.
2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa.
Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba*Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi, na kwa Al-Masihi Isa, Bwana wetu.
Shukrani na kutiwa moyo
3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. 4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha. 5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike, na ninasadiki sasa wewe pia unayo.
6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. 7 Maana Mungu hakutupatia roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.
8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema, bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Al-Masihi Isa tangu milele. 10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Al-Masihi Isa, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kupitia kwa Injili. 11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. 12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.
13 Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Al-Masihi Isa. 14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho wa Mungu akaaye ndani yetu.
15 Unajua ya kuwa watu wote katika jimbo la Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene.
16 Bwana Isa akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara, wala hakuionea aibu minyororo yangu. 17 Badala yake, alipokuwa Rumi alinitafuta kwa bidii hadi akanipata. 18 Bwana Isa na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso.
*1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.