2
Askari mwema wa Al-Masihi Isa
1 Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Al-Masihi Isa. 2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile. 3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Al-Masihi Isa. 4 Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari. 5 Vivyo hivyo, mwanariadha hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano. 6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. 7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Mwenyezi Mungu atakupa ufahamu katika mambo haya yote.
8 Mkumbuke Isa Al-Masihi aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, 9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. 10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Al-Masihi Isa, pamoja na utukufu wa milele.
11 Hili ni neno la kuaminiwa:
Kama tumekufa pamoja naye,
tutaishi pia pamoja naye.
12 Kama tukistahimili,
pia tutatawala pamoja naye.
Kama tukimkana,
naye atatukana.
13 Tusipoaminika,
yeye hudumu akiwa mwaminifu,
kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.
Mtendakazi aliyekubaliwa na Mwenyezi Mungu
14 Endelea kuwakumbusha mambo haya, ukiwaonya mbele za Mungu waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote, bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. 15 Jitahidi kujionesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. 16 Jiepushe na maneno machafu yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kutomcha Mungu. 17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto, 18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kupita, nao hupindua imani ya baadhi ya watu. 19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Mwenyezi Mungu anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Mwenyezi Mungu na auache uovu.”
20 Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida. 21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema.
22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana Isa kwa moyo safi. 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa unajua hayo huzaa magomvi. 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana Isa kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.