5
Anania na Safira
1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. 2 Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.
3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho wa Mungu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja, si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, je, fedha ulizozipata, si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.”
5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. 6 Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakampeleka nje kumzika.
7 Muda wa saa tatu baadaye, mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. 8 Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”
9 Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakupeleka nje.”
10 Wakati ule ule, akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. 11 Hofu kuu ikalipata kundi la waumini wa Isa lote, pamoja na watu wote waliosikia kuhusu matukio haya.
Mitume waponya watu wengi
12 Mitume walifanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Waumini wote walikuwa wakikusanyika katika Ukumbi wa Sulemani. 13 Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao, ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. 14 Hata hivyo, waliomwamini Bwana Isa wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake. 15 Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16 Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.
Mitume washtakiwa
17 Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo*Kundi la kidini la Wayahudi; waliamini kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho., wakajawa na wivu. 18 Wakawakamata mitume na kuwafunga gerezani. 19 Lakini wakati wa usiku, malaika wa Mwenyezi Mungu akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia, 20 “Nendeni, mkasimame Hekaluni, mkawaambie watu maneno yote ya maisha haya mapya.”
21 Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu.
Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya Baraza la Wayahudi, yaani wazee wote wa Israeli. Wakatumana wale mitume waletwe kutoka gerezani. 22 Lakini wale walinzi wa Hekalu walipoenda gerezani hawakuwakuta mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari. 23 Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na askari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu yeyote.” 24 Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.
25 Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu mliowafunga gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.” 26 Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na askari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.
27 Waliwaleta mitume, wakawasimamisha mbele ya Baraza la Wayahudi ili kuhani mkuu awahoji. 28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30 Mungu wa baba zetu alimfufua Isa kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu wa Mungu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”
33 Wale wajumbe wa Baraza la Wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua mitume. 34 Lakini Farisayo†Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa Torati, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya Baraza la Wayahudi, akaamuru mitume watolewe nje kwa muda. 35 Ndipo alipowaambia wazee wa Baraza, “Enyi wanaume wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa. 36 Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao mia nne walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu. 37 Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika. 38 Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waachieni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa. 39 Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”
40 Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Isa, wakawaachia waende zao.
41 Nao mitume wakatoka nje ya Baraza la Wayahudi, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Isa. 42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri Habari Njema kwamba Isa ndiye Al-Masihi‡Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta..
*5:17 Kundi la kidini la Wayahudi; waliamini kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho.
†5:34 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.
‡5:42 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.