Mateso na kuenea kwa Injili
6
(Matendo 6:1–9:31)
Saba wachaguliwa kuhudumu
Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, Wayahudi wa Kiyunani*Wayahudi waliofuata lugha na desturi za Kiyunani walinung’unika dhidi ya WaebraniaWayahudi walioshikilia lugha na desturi zao za Kiebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawo wa chakula wa kila siku. Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu wa Mungu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, nasi tutatumia muda wetu kuomba na katika huduma ya neno.”
Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho wa Mungu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao kutoka Antiokia, mtu wa Mataifa aliyeongokea dini ya Kiyahudi. Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono.
Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu, hata makuhani wengi wakaitii ile imani.
Kukamatwa kwa Stefano
Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa SinagogiNyumba ya ibada na mafunzo. la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa) la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na jimbo la Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. 10 Lakini hawakuweza kushindana na ile hekima aliyopewa na Roho wa Mungu alipokuwa akisema.
11 Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Musa na dhidi ya Mungu.”
Stefano afikishwa mbele ya Baraza
12 Wakawachochea watu, wazee na walimu wa Torati, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya Baraza la Wayahudi§Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.. 13 Wakawaleta mashahidi wa uongo ambao walishuhudia, wakasema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Torati. 14 Kwa maana tumemsikia akisema kwamba Isa Al-Nasiri atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Musa.”
15 Watu wote waliokuwa wameketi katika Baraza la Wayahudi wakamkazia macho Stefano, wakaona uso wake unang’aa kama uso wa malaika.

*6:1 Wayahudi waliofuata lugha na desturi za Kiyunani

6:1 Wayahudi walioshikilia lugha na desturi zao za Kiebrania

6:9 Nyumba ya ibada na mafunzo.

§6:12 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.