21
Paulo aenda Yerusalemu
1 Tulipokwisha kujitenga nao, tukasafiri kwa meli moja kwa moja hadi Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo, na kutoka huko tukaenda Patara. 2 Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo. 3 Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri hadi Siria. Tukatia nanga katika bandari ya Tiro, ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake. 4 Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wa Mungu wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. 5 Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba. 6 Baada ya kuagana, tukapanda kwenye meli, nao wakarudi manyumbani mwao.
7 Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja. 8 Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani mwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake. 9 Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.
10 Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo akateremka kutoka Yudea. 11 Alipotufikia, akachukua mshipi wa Paulo, akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe, akasema, “Roho wa Mungu anasema: ‘Hivi ndivyo viongozi wa Wayahudi huko Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’ ”
12 Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Isa.” 14 Alipokataa kushawishika, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na yatendeke.”
15 Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu. 16 Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani mwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.
Kukamatwa kwa Paulo, na safari yake kwenda Rumi
(Matendo 21:17–28:31)
Paulo awasili Yerusalemu
17 Tulipofika Yerusalemu, ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18 Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulienda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwako. 19 Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.
20 Baada ya kusikia mambo haya, wakamsifu Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria. 21 Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote wanaoishi miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Musa, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu. 22 Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu. 23 Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tuna watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. 24 Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria. 25 Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
26 Ndipo kesho yake Paulo akaenda na wale watu, akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
Paulo akamatwa
27 Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka jimbo la Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata. 28 Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.” 29 (Walikuwa wamemwona Trofimo Mwefeso, akiwa mjini pamoja na Paulo, wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)
30 Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa. 31 Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari Warumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko. 32 Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari, wakakimbia kwenye ule umati wa watu. Wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.
33 Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini. 34 Baadhi ya watu katika umati ule wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya taharuki, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi. 35 Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za umati ule wa watu zilikuwa kubwa. 36 Umati wa watu waliofuata waliendelea kupaza sauti na kusema, “Mwondoe huyu!”
Paulo anajitetea
37 Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?”
Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani? 38 Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi elfu nne wenye silaha jangwani?”
39 Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi kutoka Tarso huko Kilikia, raia wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”
40 Baada ya kupata ruhusa kwa yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi, akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema: