22
Ushuhuda wa Paulo kwa Wayahudi wa Yerusalemu
1 “Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu.”
2 Waliposikia akisema kwa lugha ya Kiebrania, wakanyamaza kabisa.
Ndipo Paulo akasema, 3 “Mimi ni Myahudi, niliyezaliwa Tarso huko Kilikia, lakini nimelelewa katika mji huu. Miguuni mwa Gamalieli, nilifundishwa kikamilifu katika sheria ya baba zetu, na nikawa mwenye juhudi kwa ajili ya Mungu kama nyote mlivyo leo. 4 Niliwatesa wafuasi wa Njia hii hadi kufa, nikiwakamata wanaume na wanawake, na kuwatupa gerezani, 5 kama kuhani mkuu na baraza zima la wazee wanavyoweza kushuhudia kunihusu. Hata nilipokea barua kutoka kwao kwenda kwa ndugu wale wa Dameski, nami nikaenda huko ili kuwaleta watu hawa Yerusalemu kama wafungwa ili waadhibiwe.
Paulo aeleza juu ya kuokoka kwake
(Matendo 9:1-19; 26:12-18)
6 “Nilipokuwa njiani kuelekea Dameski, yapata saa sita mchana, ghafula nuru kubwa kutoka mbinguni ikanimulika kotekote. 7 Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli! Sauli! Mbona unanitesa?’
8 “Nikajibu, ‘Wewe ni nani, Bwana?’
“Naye akaniambia, ‘Mimi ni Isa Al-Nasiri unayemtesa.’ 9 Basi wale watu waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia sauti ya yule aliyekuwa akisema nami.
10 “Nikauliza, ‘Nifanye nini, Bwana?’
“Naye Bwana Isa akaniambia, ‘Inuka uingie Dameski, huko utaambiwa yote unayopaswa kufanya.’ 11 Kwa kuwa nilikuwa siwezi kuona kwa ajili ya mng’ao wa ile nuru, wenzangu wakanishika mkono wakaniongoza kuingia Dameski.
12 “Mtu mmoja mcha Mungu, jina lake Anania, alikuja kuniona. Alizishika sana sheria zetu, na aliheshimiwa sana na Wayahudi walioishi huko Dameski. 13 Akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Sauli, pata kuona tena!’ Nami mara hiyo nikaweza kumwona.
14 “Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe ili ujue mapenzi yake, umwone yeye Aliye Mwenye Haki na upate kusikia maneno kutoka kinywani mwake. 15 Kwa kuwa utakuwa shahidi wake kwa watu kuhusu kile ulichokiona na kukisikia. 16 Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita Jina lake.’
Paulo atumwa kwa watu wa Mataifa
17 “Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula, 18 nikamwona Bwana Isa akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu.’
19 “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyoenda kwenye kila sinagogi*Nyumba ya ibada na mafunzo. ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini. 20 Damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’
21 “Ndipo Bwana Isa akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ”
Paulo na jemadari wa Kirumi
22 Umati ule wa watu wakamsikiliza Paulo hadi aliposema neno hilo, ndipo wakapaza sauti zao na kupiga kelele wakisema, “Mwondoeni duniani, hafai kuishi!”
23 Walipokuwa wakipiga kelele na kutoa mavazi yao huku wakirusha mavumbi juu hewani, 24 yule jemadari akaamuru Paulo aingizwe kwenye ngome. Akaelekeza kwamba apigwe mijeledi na ahojiwe ili kujua kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna hiyo. 25 Lakini walipokwisha kumfunga kwa kamba za ngozi ili wampige mijeledi, Paulo akamwambia kiongozi wa askari aliyekuwa amesimama pale karibu naye, “Je, ni halali kwenu kwa mujibu wa sheria kumpiga mtu ambaye ni raia wa Rumi hata kabla hajapatikana na hatia?”
26 Yule kiongozi aliposikia maneno haya, alimwendea yule jemadari na kumwambia, “Unataka kufanya nini? Kwa maana huyu mtu ni raia wa Rumi.”
27 Yule jemadari akaja akamuuliza Paulo, “Niambie, wewe ni raia wa Rumi?”
Paulo akajibu, “Naam, hakika.”
28 Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.”
Paulo akasema “Lakini mimi ni raia wa Rumi kwa kuzaliwa.”
29 Mara wale waliokuwa wanataka kumhoji wakajiondoa haraka, naye yule jemadari akaingiwa na hofu alipotambua ya kuwa amemfunga Paulo, ambaye ni raia wa Rumi, kwa minyororo.
Paulo apelekwa mbele ya Baraza
30 Kesho yake, kwa kuwa yule jemadari alitaka kujua hakika kwa nini Paulo alikuwa anashutumiwa na Wayahudi, alimfungua, na akawaagiza viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi†Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. lote likutane. Kisha akamleta Paulo, akamsimamisha mbele yao.