5
Maombolezo na wito wa toba 
  1 Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:   
 2 “Bikira Israeli ameanguka,  
kamwe hatainuka tena,  
ameachwa pweke katika nchi yake,  
hakuna yeyote wa kumwinua.”   
 3 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:  
“Mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli,  
mia moja tu watarudi;  
wakati mji utakapopeleka mia moja,  
kumi tu ndio watarudi hai.”   
 4 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa nyumba ya Israeli:  
“Nitafuteni mpate kuishi;   
 5 msitafute Betheli,  
msiende Gilgali,  
msisafiri kwenda Beer-Sheba.  
Kwa maana kwa hakika Gilgali itaenda uhamishoni,  
na Betheli itafanywa kuwa ubatili*yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni (taz. Hosea 4:15)..”   
 6 Mtafuteni Mwenyezi Mungu mpate kuishi,  
au atafagia nyumba ya Yusufu kama moto;  
utawateketeza, nayo Betheli  
haitakuwa na yeyote wa kuuzima.   
 7 Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu  
na kuiangusha haki chini   
 8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,  
ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko  
na mchana kuwa usiku,  
ambaye huyaita maji ya bahari  
na kuyamwaga juu ya nchi:  
Mwenyezi Mungu ndilo jina lake;   
 9 yeye hufanya maangamizi kwenye ngome  
na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),   
 10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani,  
na kumdharau yule ambaye husema kweli.   
 11 Mnamgandamiza maskini  
na kumlazimisha awape nafaka.  
Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,  
hamtaishi ndani yake;  
ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,  
hamtakunywa divai yake.   
 12 Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu  
na ukubwa wa dhambi zenu.  
Mmewadhulumu wenye haki na kupokea rushwa  
na kuzuia haki ya maskini mahakamani.   
 13 Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza nyakati kama hizo,  
kwa kuwa nyakati ni mbaya.   
 14 Tafuteni mema, wala si mabaya,  
ili mpate kuishi.  
Ndipo Bwana Mwenyezi Mungu,  
Mungu wa majeshi ya mbinguni  
atakuwa pamoja nanyi,  
kama msemavyo yupo nanyi.   
 15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;  
dumisheni haki mahakamani.  
Yamkini Bwana Mwenyezi Mungu,  
Mungu wa majeshi ya mbinguni,  
atawahurumia mabaki ya Yusufu.   
 16 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, yeye Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asemalo:  
“Kutakuwa na maombolezo barabarani zote,  
na vilio vya uchungu katika njia kuu zote.  
Wakulima wataitwa kuja kulia,  
na waombolezaji waje kuomboleza.   
 17 Kutakuwa na kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,  
kwa kuwa nitapita kati yenu,”  
asema Mwenyezi Mungu.   
Siku ya Mwenyezi Mungu 
  18 Ole wenu ninyi mnaoitamani  
siku ya Mwenyezi Mungu!  
Kwa nini mnaitamani siku ya Mwenyezi Mungu?  
Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.   
 19 Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba  
kumbe akakutana na dubu,  
kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake  
na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta,  
kumbe akaumwa na nyoka.   
 20 Je, siku ya Mwenyezi Mungu haitakuwa giza, na si nuru:  
giza nene, bila mwali wowote?   
 21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;  
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.   
 22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,  
sitazikubali.  
Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,  
sitazitambua.   
 23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!  
Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.   
 24 Lakini acheni haki itiririke kama mto,  
na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!   
 25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka  
kwa miaka arobaini kule jangwani,  
ee nyumba ya Israeli?   
 26 Mmeyainua madhabahu ya Sikuthi  
mungu wenu mtawala,  
na Kiuni mungu wenu wa nyota,  
ambao mliwatengeneza wenyewe.   
 27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”  
asema Mwenyezi Mungu, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi ya mbinguni.