6
Ole kwa wanaoridhika
1 Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,
na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria,
ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,
ambao watu wa Israeli wanawategemea!
2 Nendeni Kalne mkaone kutoka huko;
mwende hadi Hamathi iliyo kuu,
kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.
Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?
Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?
3 Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya
na kuleta karibu utawala wa kuogofya.
4 Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu,
na kujinyoosha juu ya viti vya fahari.
Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri
na ndama walionenepeshwa.
5 Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi,
huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.
6 Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa,
na mnajipaka mafuta mazuri,
lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yusufu.
7 Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni;
karamu zenu na kustarehe kutakoma.
Mwenyezi Mungu anachukia kiburi cha Israeli
8 Bwana Mungu Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema:
“Nachukia kiburi cha Yakobo,
nachukia ngome zake;
nitautoa mji wao na kila kitu
kilicho ndani yake.”
9 Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa. 10 Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza! Haturuhusiwi kutaja jina la Mwenyezi Mungu.”
11 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamuru,
naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande
na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.
12 Je, farasi wanaweza kukimbia
kwenye miamba iliyochongoka?
Je, mtu aweza kulima kwa maksai huko?
Lakini mmegeuza haki kuwa sumu
na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:
13 ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari
na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu
kwa nguvu zetu wenyewe?”
14 Maana Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema,
“Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli,
nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi
hadi Bonde la Araba.”