4
Israeli waamriwa kutii
1 Sikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zako, anawapa. 2 Usiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambayo nawapa.
3 Mliona kwa macho yenu wenyewe kile Mwenyezi Mungu alichokifanya kule Baal-Peori. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori, 4 lakini ninyi nyote mlioshikamana na Mwenyezi Mungu kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai hadi leo.
5 Tazama, nimewafundisha amri na sheria kama Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki. 6 Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.” 7 Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba? 8 Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?
9 Mwe waangalifu na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke mioyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.
10 Kumbuka siku uliyosimama mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kule Horebu aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.” 11 Mlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto hadi juu mbinguni, pamoja na mawingu meusi na giza nene. 12 Ndipo Mwenyezi Mungu alipozungumza nanyi kutoka kati ya moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu. 13 Aliwatangazia agano lake, hizo Amri Kumi ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe. 14 Naye Mwenyezi Mungu alinielekeza wakati huo kuwafundisha ninyi sheria na amri ambazo mnapaswa kuzifuata katika nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki.
Kuabudu sanamu kwakatazwa
15 Hamkuona umbo la aina yoyote siku ambayo Mwenyezi Mungu alizungumza nanyi kule Horebu kutoka kati ya moto. Kwa hiyo mjihadhari kwa uangalifu sana, 16 ili msije mkajichafua na kujitengenezea sanamu au kinyago chenye umbo lolote kama la mwanaume au mwanamke, 17 au kama mnyama aliye juu ya nchi au ndege yeyote arukaye angani, 18 au kama kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi, au samaki yeyote aliye ndani ya maji. 19 Na utazamapo juu angani na ukaliona jua, mwezi na nyota na vyote vinavyoipamba mbingu, usije ukashawishiwa kuviinamia na kuviabudu vitu ambavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivigawia mataifa yote chini ya mbingu. 20 Lakini ninyi, Mwenyezi Mungu amewatoa kutoka tanuru la kuyeyushia chuma, kutoka Misri, kuwa watu wa urithi wake, kama mlivyo sasa.
21 Mwenyezi Mungu alinikasirikia kwa sababu yenu na akaapa kwamba sitavuka Yordani kuingia katika nchi nzuri Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayowapa kuwa urithi wenu. 22 Nitakufa katika nchi hii; sitavuka Yordani, lakini ninyi ni karibu mvuke mkaimiliki ile nchi nzuri. 23 Jihadharini msilisahau agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, lile alilofanya nanyi; msijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewakataza. 24 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.
25 Baada ya kuwa na watoto na wajukuu na kuishi katika nchi hiyo siku nyingi, tena mkijichafua na kutengeneza sanamu ya aina yoyote, mkifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kumfanya awe na hasira, 26 ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yenu siku hii kwamba mtaangamia mara moja kutoka katika nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki. Hamtaishi kule kwa muda mrefu bali kwa hakika mtaangamizwa. 27 Mwenyezi Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa, na ni wachache wenu tu watakaosalia miongoni mwa mataifa hayo ambayo Mwenyezi Mungu atawafukuzia. 28 Huko mtaabudu miungu ya miti na mawe iliyotengenezwa na watu, ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kula au kunusa. 29 Lakini kama mtamtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mtampata; kama mtamtafuta kwa moyo wote na kwa roho yote. 30 Mnapokuwa katika dhiki, nayo mambo haya yote yamewatokea siku hizo, ndipo mtamrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kumtii. 31 Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mungu mwenye huruma, hatawaacha au kuwaangamiza wala kusahau agano alilofanya na baba zenu, alilowathibitishia kwa kiapo.
Mwenyezi Mungu ndiye Mungu pekee
32 Sasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa? 33 Je, kuna watu wengine wowote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi? 34 Je, kuna mungu yeyote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu ya kutisha, kama yale ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu?
35 Mlioneshwa mambo haya ili mpate kujua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu; hakuna mwingine ila yeye. 36 Kutoka mbinguni amewasikizisha sauti yake ili kuwaadilisha. Hapa duniani aliwaonesha moto wake mkubwa, nanyi mlisikia maneno yake kutoka kati ya ule moto. 37 Kwa sababu aliwapenda baba zenu na alichagua wazao wao baada yao, aliwatoa katika nchi ya Misri kwa Uwepo wake na kwa uwezo wake mkuu, 38 aliwafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi na kuwaleta ninyi katika nchi yao na akawapa ninyi kuwa urithi wenu, kama ilivyo leo.
39 Kubalini na mweke moyoni leo kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu mbinguni juu na duniani chini. Hakuna mwingine. 40 Mshike amri na maagizo yake ninayowapa leo, ili mpate kufanikiwa ninyi na watoto wenu baada yenu, na mpate kuishi maisha marefu katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, siku zote.
Miji ya makimbilio
41 Kisha Musa akatenga miji mitatu mashariki mwa Yordani, 42 ambayo mtu yeyote aliyemuua mtu angeweza kukimbilia ikiwa amemuua jirani yake bila kukusudia na bila kuwa na chuki naye siku zilizopita. Angeweza kukimbilia katika mmoja ya miji hii na kuokoa maisha yake. 43 Miji hiyo ilikuwa: Bezeri katika tambarare ya jangwa kwa ajili ya Wareubeni; Ramothi katika nchi ya Gileadi kwa ajili ya Wagadi; nao mji wa Golani katika nchi ya Bashani kwa ajili ya Wamanase.
Utangulizi wa Torati
44 Hii ndiyo sheria Musa aliyoweka mbele ya Waisraeli. 45 Haya ndio masharti, amri na sheria Musa alizowapa Waisraeli walipotoka Misri, 46 nao walikuwa katika bonde karibu na Beth-Peori mashariki mwa Yordani, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni; naye alishindwa na Musa na Waisraeli walipotoka Misri. 47 Waliimiliki nchi yake na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, wafalme wawili Waamori waliotawala mashariki mwa Yordani. 48 Nchi hii ilienea kutoka Aroeri ukingoni mwa Bonde la Arnoni hadi Mlima Sioni (yaani Hermoni), 49 pamoja na eneo lote la Araba mashariki mwa Yordani, na kuenea hadi Bahari ya Araba kwenye miteremko ya Pisga.