5
Amri Kumi
(Kutoka 20:1-17)
1 Musa akawaita Israeli wote, akawaambia:
Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata. 2 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika mlima wa Horebu. 3 Si kwamba Mwenyezi Mungu alifanya agano na baba zetu, bali alifanya nasi, nasi sote ambao tuko hai hapa leo. 4 Mwenyezi Mungu alisema nanyi uso kwa uso kutoka kati ya moto juu ya mlima. 5 (Wakati huo nilisimama kati ya Mwenyezi Mungu na ninyi kuwatangazia neno la Mwenyezi Mungu, kwa sababu mliogopa ule moto, nanyi hamkupanda mlimani.)
Naye Mungu alisema:
6 “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
7 “Usiwe na miungu mingine ila mimi.
8 Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji. 9 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanaonichukia, 10 lakini ninaonesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaonipenda na kuzishika amri zangu.
11 Usilitaje bure jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
12 Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alivyokuagiza. 13 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote. 14 Lakini siku ya saba ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au wa kike, wala ng’ombe wako, punda wako au mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye malangoni mwako, ili mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika kama wewe. 15 Kumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato.
16 Waheshimu baba yako na mama yako, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anayokupa.
17 Usiue.
18 Usizini.
19 Usiibe.
20 Usimshuhudie jirani yako uongo.
21 Usitamani mke wa jirani yako. Usitamani nyumba ya jirani yako au shamba lake, mtumishi wake wa kiume au wa kike, ng’ombe au punda wake, wala kitu chochote cha jirani yako.”
22 Hizi ndizo amri alizozitangaza Mwenyezi Mungu kwa sauti kubwa kwa kusanyiko lenu lote huko mlimani kutoka kati ya moto na wingu na giza nene, wala hakuongeza chochote zaidi. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, naye akanipa mimi.
Woga wa watu mlimani
(Kutoka 20:18-21)
23 Mliposikia sauti kutoka kati ya giza, mlima ulipokuwa ukiwaka moto, viongozi wenu wote wa makabila yenu na wazee wenu walinijia mimi. 24 Nanyi mkasema, “Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ametuonesha utukufu na enzi yake, nasi tumesikia sauti yake kutoka kati ya moto. Leo tumeona kwamba mwanadamu anaweza kuishi hata kama Mungu akizungumza naye. 25 Lakini sasa, kwa nini tufe? Moto huu mkubwa utatuteketeza sisi na tutakufa tukiendelea kusikia sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, zaidi. 26 Ni mtu yupi mwenye mwili ambaye amewahi kuisikia sauti ya Mungu aliye hai akizungumza kutoka kati ya moto, kama sisi tulivyoisikia, naye akaishi? 27 Sogea karibu usikie yale yote asemayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Kisha utuambie chochote kile ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anakuambia. Tutasikiliza na kutii.”
28 Mwenyezi Mungu aliwasikia wakati mlipozungumza nami, na Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nimesikia kile hawa watu walichokuambia. Kila kitu walichokisema ni kizuri. 29 Laiti kama mioyo yao ingekuwa na mwelekeo wa kuniogopa na kuzishika amri zangu zote daima, ili wafanikiwe wao pamoja na watoto wao milele!
30 “Nenda uwaambie warudi kwenye mahema yao. 31 Lakini wewe baki hapa pamoja nami ili niweze kukupa maagizo yote, amri na sheria ambazo utawafundisha wazifuate katika nchi ninayoenda kuwapa waimiliki.”
32 Hivyo kuweni waangalifu kuyafanya yale Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyowaagiza; msigeuke upande wa kuume wala wa kushoto. 33 Fuateni yale yote ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaagiza, ili mpate kuishi, kustawi na kuziongeza siku zenu katika nchi mtakayoimiliki.