9
Si kwa sababu ya haki ya Waisraeli
(Kutoka 32:1-35)
1 Sikiliza, ee Israeli. Sasa mnakaribia kuvuka Yordani mwingie na kuwafukuza mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi pamoja na miji mikubwa yenye kuta zilizofika juu angani. 2 Watu ni wenye nguvu na warefu, ni wana wa Waanaki! Mnafahamu habari zao na mmesikia inavyosemekana: “Ni nani awezaye kusimama dhidi ya Waanaki?” 3 Kuweni na hakika leo kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayetangulia kuvuka mbele yenu kama moto uteketezao. Atawaangamiza; atawatiisha mbele yenu. Nanyi mtawafukuza na kuwaangamiza mara moja, kama Mwenyezi Mungu alivyowaahidi.
4 Baada ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kuwafukuza mbele yenu, msiseme mioyoni mwenu, “Mwenyezi Mungu ametuleta hapa kuimiliki nchi hii kwa sababu ya haki yetu.” La, ni kwa sababu ya uovu wa mataifa haya ndio Mwenyezi Mungu anawafukuza mbele yenu. 5 Si kwa sababu ya haki yenu wala uadilifu wenu kwamba mtaimiliki nchi yao; lakini kwa sababu ya uovu wa mataifa haya, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawafukuza mbele yenu, ili kutimiza lile alilowaapia baba zenu Ibrahimu, Isaka na Yakobo. 6 Basi mjue, si kwa sababu ya haki yenu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa nchi hii nzuri kuimiliki, kwa kuwa ninyi ni taifa lenye shingo ngumu.
Ndama ya dhahabu
7 Kumbukeni hili, kamwe msisahau jinsi mlivyomkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa hasira huko jangwani. Tangu siku mlipotoka Misri hadi mlipofika hapa, mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi Mungu. 8 Kule Horebu mliamsha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo alikasirika sana hata akataka kuwaangamiza. 9 Nilipopanda mlimani kupokea vibao vya mawe, vile vibao vya agano ambalo Mwenyezi Mungu alilifanya nanyi, nilikaa mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula mkate wala sikunywa maji. 10 Mwenyezi Mungu alinipa vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu. Juu ya vibao hivyo kulikuwa amri zote Mwenyezi Mungu alizowatangazia kule mlimani kutoka kati ya moto siku ya kusanyiko.
11 Mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, Mwenyezi Mungu alinipa vibao viwili vya mawe, vile vibao vya agano. 12 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Shuka chini mara moja, kwa sababu watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamepotoka. Wamegeukia mbali haraka kutoka lile nililowaagiza, wamejitengenezea sanamu ya kusubu.”
13 Naye Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nimewaona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu sana! 14 Niache, ili nipate kuwaangamiza na kufuta jina lao chini ya mbingu. Nami nitakufanya kuwa taifa lenye nguvu zaidi na kuwa wengi kuliko wao.”
15 Kwa hiyo, niligeuka na kuteremka kutoka mlimani kwani mlima ulikuwa ukiwaka moto. Pia vile vibao viwili vya agano vilikuwa mikononi mwangu. 16 Nilipotazama, niliona kuwa mmefanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; mmejifanyia sanamu ya kusubu katika umbo la ndama. Mmegeuka upesi kutoka njia ile Mwenyezi Mungu aliyowaagiza. 17 Kwa hiyo nilichukua vile vibao viwili, nikavitupa na kuvipasua vipande vipande mbele ya macho yenu.
18 Ndipo tena nikasujudu hadi chini mbele za Mwenyezi Mungu kwa siku arobaini usiku na mchana. Sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi yote mliyoifanya, mkifanya lile lililo ovu mbele za Mwenyezi Mungu na kumkasirisha. 19 Niliogopa hasira na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa aliwakasirikia ninyi sana na kutaka kuwaangamiza. Bali Mwenyezi Mungu alinisikiliza tena. 20 Lakini Mwenyezi Mungu alimkasirikia Haruni kiasi cha kutaka kumwangamiza, nami wakati huo nilimwombea Haruni pia. 21 Kisha nikachukua ile sanamu ya ndama mliyoitengeneza na kuichoma kwenye moto. Nikaiponda na kuisaga ikawa unga laini kama vumbi, nikatupa lile vumbi kwenye kijito kilichotiririka toka mlimani.
22 Pia mlimkasirisha Mwenyezi Mungu huko Tabera, Masa na Kibroth-Hataava.
23 Vilevile wakati Mwenyezi Mungu alipowatuma kutoka Kadesh-Barnea, alisema, “Kweeni, mkaimiliki nchi niliyowapa.” Lakini mliasi dhidi ya agizo la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Hamkumtegemea wala kumtii. 24 Mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi Mungu tangu nilipowajua ninyi.
25 Nilianguka kifudifudi mbele za Mwenyezi Mungu kwa zile siku arobaini usiku na mchana kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amesema angewaangamiza ninyi. 26 Nilimwomba Mwenyezi Mungu na kusema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, usiangamize watu wako, urithi wako mwenyewe ule ulioukomboa kwa uweza wako mkuu na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu. 27 Wakumbuke watumishi wako Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Usiangalie ukaidi wa watu hawa, uovu wao wala dhambi yao. 28 Watu wa nchi ile uliyotutoa sisi wasije wakasema, ‘Ni kwa sababu Mwenyezi Mungu hakuweza kuwachukua hadi nchi aliyokuwa amewaahidia, kwa sababu aliwachukia, akawaleta ili aje kuwaua jangwani.’ 29 Bali wao ni watu wako, urithi wako ule ulioutoa Misri kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyooka.”