10
Vibao Vingine vya Amri Kumi
(Kutoka 34:1-10)
Wakati ule Mwenyezi Mungu aliniambia, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza uje kwangu juu mlimani. Pia utengeneze Sanduku la mbao. Nitaandika juu ya vibao maneno yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza, ambavyo ulivivunja. Kisha utaviweka ndani ya Sanduku.”
Hivyo nikatengeneza Sanduku kwa mti wa mshita, nikachonga pia vibao vya mawe kama vile vya kwanza, kisha nikakwea mlimani nikiwa na vile vibao viwili mikononi mwangu. Mwenyezi Mungu akaandika juu ya hivi vibao kile alichokuwa amekiandika kabla, Amri Kumi alizokuwa amewatangazia huko mlimani, kutoka kati ya moto siku ile ya kusanyiko. Mwenyezi Mungu akanikabidhi. Kisha nikashuka kutoka mlimani na kuweka vibao ndani ya Sanduku nililokuwa nimelitengeneza, kama Mwenyezi Mungu alivyoniagiza, navyo viko huko sasa.
(Waisraeli walisafiri kutoka visima vya Bene-Yaakani hadi Mosera. Huko Haruni alifariki na kuzikwa, naye Eleazari mwanawe akachukua nafasi yake kama kuhani. Kutoka pale, walisafiri hadi Gudgoda wakaendelea hadi Yotbatha, nchi yenye vijito vya maji. Wakati huo Mwenyezi Mungu aliteua kabila la Lawi kulibeba Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, kusimama mbele za Mwenyezi Mungu ili kutoa huduma, na kutangaza baraka kwa Jina lake, kama wanavyofanya hadi leo. Hiyo ndiyo sababu ya Walawi kutokuwa na sehemu wala urithi miongoni mwa ndugu zao; Mwenyezi Mungu ndiye urithi wao, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wao, alivyowaambia.)
10 Basi nilikaa mlimani kwa siku arobaini usiku na mchana, kama nilivyofanya mara ya kwanza, pia Mwenyezi Mungu alinisikiliza hata wakati huu. Haikuwa nia yake kuwaangamiza. 11 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nenda, ukawaongoze watu katika njia yao ili waweze kuingia na kuimiliki nchi ile niliyowaapia baba zao kuwapa.”
Mche Mwenyezi Mungu
12 Na sasa, ee Israeli, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anataka nini kwako ila kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, 13 na kuyashika maagizo ya Mwenyezi Mungu na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?
14 Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo, ni mali ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. 15 Hata hivyo Mwenyezi Mungu alikuwa na shauku na baba zako, akawapenda na akawachagua ninyi, wazao wao, kuliko mataifa yote, kama ilivyo leo. 16 Kwa hiyo tahirini mioyo yenu, na msiwe na shingo ngumu tena. 17 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa. 18 Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. 19 Nanyi wapendeni wageni, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni huko Misri. 20 Mche Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye. Shikamana naye kwa uthabiti na kuapa kwa jina lake. 21 Yeye ni sifa yako; yeye ni Mungu wako, ambaye alikutendea yale maajabu makubwa na ya kutisha uliyoyaona kwa macho yako mwenyewe. 22 Baba zako walioshuka kwenda Misri jumla yao walikuwa sabini, na sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekufanya taifa la watu wengi kama nyota za angani.