31
Yoshua kutawala baada ya Musa
(Hesabu 27:12-23)
1 Kisha Musa akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote: 2 “Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. Mwenyezi Mungu ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’ 3 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama Mwenyezi Mungu alivyosema. 4 Naye Mwenyezi Mungu atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao. 5 Mwenyezi Mungu atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mkawatendee yale yote niliyowaamuru. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anaenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”
7 Kisha Musa akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Mwenyezi Mungu aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8 Mwenyezi Mungu mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”
Kusoma Torati
9 Kwa hiyo Musa akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na wazee wote wa Israeli. 10 Kisha Musa akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, 11 Waisraeli wote wanapokuja mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. 12 Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuzingatia maneno yote ya sheria hii. 13 Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
Kuasi kwa Waisraeli kunatabiriwa
14 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sasa siku ya kifo chako imekaribia. Mwite Yoshua, mkajihudhurishe katika Hema la Kukutania, mahali nitakapompa maagizo ya kazi.” Kwa hiyo Musa na Yoshua wakaja na kujihudhurisha kwenye Hema la Kukutania.
15 Kisha Mwenyezi Mungu akatokea katika Hema katika nguzo ya wingu, nalo wingu likasimama juu ya ingilio la Hema. 16 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: “Unaenda kupumzika na baba zako, nao watu hawa hivi karibuni watazini na miungu migeni ya nchi wanayoingia. Wataniacha na kuvunja agano nililofanya nao. 17 Siku hiyo nitawakasirikia na kuwaacha; nitawaficha uso wangu, nao wataangamizwa. Maafa mengi na shida nyingi zitakuja juu yao, nao siku hiyo watauliza, ‘Je, maafa haya hayakuja juu yetu kwa sababu Mungu wetu hayuko pamoja nasi?’ 18 Nami hakika nitauficha uso wangu siku hiyo kwa sababu ya maovu yao yote kwa kugeukia miungu mingine.
19 “Sasa ujiandikie wimbo huu, uwafundishe Waisraeli na uwaamuru wauimbe, ili upate kuwa ushahidi wangu dhidi yao. 20 Nitakapokwisha kuwaingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja agano langu. 21 Maafa na shida zitakapokuja juu yao, wimbo huu utashuhudia dhidi yao, kwa sababu hautasahauliwa na wazao wao. Ninajua lile wanaloandaa kufanya, hata kabla sijawaingiza katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo.” 22 Hivyo Musa akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.
23 Mwenyezi Mungu akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”
24 Baada ya Musa kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho, 25 akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu agizo hili, akawaambia: 26 “Chukueni Kitabu hiki cha Torati mkakiweke kando ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu. 27 Kwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi ya Mwenyezi Mungu nikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu! 28 Kusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao. 29 Kwa kuwa ninajua, baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata, kwa sababu mtafanya maovu mbele za macho ya Mwenyezi Mungu, na kuchochea hasira yake kwa kazi za mikono yenu.”
Wimbo wa Musa
30 Musa akayasoma maneno ya wimbo huu kutoka mwanzo hadi mwisho katika masikio ya kusanyiko lote la Israeli: