32
Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitasema;
sikia, ee nchi, maneno ya kinywa changu.
Mafundisho yangu na yanyeshe kama mvua,
na maneno yangu na yashuke kama umande,
kama manyunyu juu ya majani mabichi,
kama mvua tele juu ya mimea myororo.
 
Nitalitangaza jina la Mwenyezi Mungu.
Naam, sifuni ukuu wa Mungu wetu!
Yeye ni Mwamba, kazi zake ni kamilifu,
njia zake zote ni haki.
Mungu mwaminifu ambaye hakosei,
yeye ni mnyofu na mwenye haki.
 
Wamefanya mambo ya upotovu mbele zake;
kwa aibu yao, wao si watoto wake tena,
lakini ni kizazi kilicho kiovu na kilichopotoka.
Je, hii ndiyo njia ya kumlipa Mwenyezi Mungu,
enyi watu wajinga na wasio na busara?
Je, yeye siye Baba yenu, Muumba wenu,
aliyewafanya ninyi na kuwaumba?
 
Kumbuka siku za kale;
tafakari vizazi vya zamani vilivyopita.
Uliza baba yako, naye atakuambia,
wazee wako, nao watakueleza.
Aliye Juu Sana alipowapa mataifa urithi wao,
alipogawanya wanadamu wote,
aliweka mipaka kwa ajili ya mataifa
sawasawa na hesabu ya wana wa Israeli.
Kwa kuwa fungu la Mwenyezi Mungu ni watu wake,
Yakobo kura yake ya urithi.
 
10 Katika nchi ya jangwa alimkuta,
katika nyika tupu ivumayo upepo.
Alimhifadhi na kumtunza;
akamlinda kama mboni ya jicho lake,
11 kama tai avurugaye kiota chake,
na kurukaruka juu ya makinda yake,
ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka,
na huwachukua kwenye mabawa yake.
12 Mwenyezi Mungu peke yake alimwongoza;
hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.
 
13 Akamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi,
akamlisha kwa mavuno ya mashamba.
Akamlea kwa asali toka mwambani,
na kwa mafuta kutoka mwamba wa gumegume,
14 kwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ng’ombe
na kutoka makundi ya mbuzi,
kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi,
kwa kondoo dume wazuri wa Bashani,
na kwa ngano nzuri.
Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.
 
15 Yeshuruni*maana yake Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli alinenepa na kupiga teke;
alikuwa na chakula tele,
akawa mzito na akapendeza sana.
Akamwacha Mungu aliyemuumba,
na kumkataa Mwamba Mwokozi wake.
16 Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni,
na kumkasirisha kwa sanamu zao
za machukizo.
17 Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu:
miungu wasiyoijua,
miungu iliyojitokeza siku za karibuni,
miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.
18 Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi;
mkamsahau Mungu aliyewazaa.
 
19 Mwenyezi Mungu akaona hili, akawakataa,
kwa sababu alikasirishwa
na wanawe wa kiume na wa kike.
20 Akasema, “Nitawaficha uso wangu,
nami nione mwisho wao utakuwa nini,
kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka,
watoto ambao si waaminifu.
21 Wamenifanya niwe na wivu
kwa kile ambacho si mungu,
na kunikasirisha
kwa sanamu zao batili.
Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa.
Nitawafanya wakasirishwe
na taifa lile lisilo na ufahamu.
22 Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu,
ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti.
Utateketeza dunia pamoja na mazao yake,
na kuwasha moto katika misingi ya milima.
 
23 “Nitalundika majanga juu yao
na kutumia mishale yangu dhidi yao.
24 Nitatuma njaa ya kudhoofisha dhidi yao,
maradhi mabaya yateketezayo,
na tauni ya kufisha;
nitawapelekea wanyama mwitu wenye meno makali,
na nyoka wenye sumu watambaao mavumbini.
25 Barabarani upanga utawakosesha watoto;
nyumbani mwao hofu itatawala.
Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia,
pia watoto wachanga na wazee wenye mvi.
26 Nilisema ningewatawanya
na kufuta kumbukumbu lao
katika mwanadamu.
27 Lakini nilihofia dhihaka za adui,
adui asije akashindwa kuelewa,
na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda;
Mwenyezi Mungu hakufanya haya yote.’ ”
 
28 Wao ni taifa lisilo na akili,
hakuna busara ndani yao.
29 Laiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili,
na kutambua mwisho wao utakuwaje!
30 Mtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja,
au wawili kufukuza elfu kumi,
kama si kwamba Mwamba wao amewauza,
kama si kwamba Mwenyezi Mungu amewaacha?
31 Kwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu,
sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri.
32 Mzabibu wao unatoka mzabibu wa Sodoma,
na kutoka mashamba ya Gomora.
Zabibu zake zimejaa sumu,
na vishada vyake vimejaa uchungu.
33 Mvinyo wao ni sumu ya nyoka,
sumu yenye kufisha ya swila.
 
34 “Je, hili sikuliweka akiba
na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina?
35 Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.
Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza;
siku yao ya maafa ni karibu,
na maangamizi yao yanawajia haraka.”
 
36 Mwenyezi Mungu atawahukumu watu wake,
na kuwahurumia watumishi wake
atakapoona nguvu zao zimekwisha
wala hakuna yeyote aliyebaki,
mtumwa au aliye huru.
37 Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao,
mwamba walioukimbilia,
38 miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao
na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji?
Wainuke basi, wawasaidie!
Wawapeni basi ulinzi!
 
39 “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye!
Hakuna mungu mwingine ila Mimi.
Mimi ninaua na Mimi ninafufua,
Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya,
wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.
40 Ninainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema:
Hakika kama niishivyo milele,
41 wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta
na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu,
nitalipiza kisasi juu ya adui zangu
na kuwalipiza wale wanaonichukia.
42 Nitailevya mishale yangu kwa damu,
wakati upanga wangu ukitafuna nyama:
damu ya waliochinjwa pamoja na mateka,
vichwa vya viongozi wa adui.”
 
43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake,
kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake,
atalipiza kisasi juu ya adui zake
na kufanya upatanisho
kwa ajili ya nchi na watu wake.
44 Musa na Yoshuayaani Yehoshea kwa Kiebrania, maana yake Yehova ni Mwokozi mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia. 45 Musa alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote, 46 akawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii. 47 Siyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
Musa aelezwa kifo chake
48 Siku hiyo hiyo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 49 “Kwea katika safu za Abarimu hadi kilima cha Nebo kilicho Moabu, ng’ambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe. 50 Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Haruni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake. 51 Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli. 52 Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”

*32:15 maana yake Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli

32:44 yaani Yehoshea kwa Kiebrania, maana yake Yehova ni Mwokozi