33
Musa anayabariki makabila 
  1 Hii ndiyo baraka Musa mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake.   2 Alisema:  
“Mwenyezi Mungu alikuja kutoka Mlima Sinai,  
akachomoza kama jua juu yao  
kutoka Mlima Seiri,  
akaangaza kutoka Mlima Parani.  
Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu  
kutoka kusini,  
kutoka miteremko ya mlima wake.   
 3 Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu,  
watakatifu wako wote wamo mkononi mwako.  
Miguuni pako wote wanasujudu,  
na kutoka kwako wanapokea mafundisho,   
 4 sheria ile Musa aliyotupatia sisi,  
tulio milki ya kusanyiko la Yakobo.   
 5 Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni*maana yake Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli  
wakati viongozi wa watu walipokusanyika,  
pamoja na makabila ya Israeli.   
 6 “Reubeni na aishi, asife,  
wala watu wake wasiwe wachache.”   
 7 Akasema hili kuhusu Yuda:  
“Ee Mwenyezi Mungu, sikia kilio cha Yuda,  
mlete kwa watu wake.  
Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea.  
Naam, uwe msaada wake  
dhidi ya adui zake!”   
 8 Kuhusu Lawi alisema:  
“Thumimu yako na Urimu†Thumimu na Urimu maana yake Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha kifuani cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha. yako ulimpa,  
mtu yule uliyemfadhili.  
Ulimjaribu huko Masa  
na kushindana naye  
kwenye maji ya Meriba.   
 9 Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake,  
‘Mimi siwahitaji kamwe.’  
Akawasahau jamaa zake,  
asiwatambue hata watoto wake,  
lakini akaliangalia neno lako  
na kulilinda agano lako.   
 10 Humfundisha Yakobo mausia yako  
na Israeli sheria yako.  
Hufukiza uvumba mbele zako  
na sadaka nzima za kuteketezwa  
juu ya madhabahu yako.   
 11 Ee Mwenyezi Mungu, bariki ustadi wake wote,  
nawe upendezwe na kazi ya mikono yake.  
Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake;  
wapige adui zake hata wasiinuke tena.”   
 12 Kuhusu Benyamini akasema:  
“Mwache mpendwa wa Mwenyezi Mungu  
apumzike salama kwake,  
kwa maana humkinga mchana kutwa,  
na yule Mwenyezi Mungu ampendaye  
hupumzika kati ya mabega yake.”   
 13 Kuhusu Yusufu akasema:  
“Mwenyezi Mungu na aibariki nchi yake  
kwa umande wa thamani  
kutoka juu mbinguni,  
na vilindi vya maji  
vilivyotulia chini;   
 14 pamoja na vitu vilivyo bora sana  
viletwavyo na jua,  
na vitu vizuri sana vinavyoweza  
kutolewa na mwezi;   
 15 pamoja na zawadi bora sana  
za milima ya zamani  
na kwa wingi wa baraka  
za vilima vya milele;   
 16 pamoja na baraka nzuri mno  
za ardhi na ukamilifu wake,  
na upendeleo wake yeye  
aliyeishi kwenye kichaka  
kilichokuwa kinawaka moto.  
Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yusufu,  
juu ya paji la uso la aliye mkuu  
miongoni mwa ndugu zake.   
 17 Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza;  
pembe zake ni pembe za nyati,  
na kwa pembe hizo atapiga mataifa,  
hata yaliyo miisho ya dunia.  
Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu;  
hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.”   
 18 Kuhusu Zabuloni akasema:  
“Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje,  
nawe Isakari, katika mahema yako.   
 19 Watawaita mataifa kwenye mlima,  
na huko mtatoa dhabihu za haki;  
watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari,  
kwa hazina zilizofichwa mchangani.”   
 20 Kuhusu Gadi akasema:  
“Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi!  
Gadi huishi huko kama simba,  
akirarua kwenye mkono au kichwa.   
 21 Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote  
kwa ajili yake mwenyewe;  
fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa  
kwa ajili yake.  
Viongozi wa watu walipokusanyika,  
alitimiza haki ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu,  
na hukumu zake kuhusu Israeli.”   
 22 Kuhusu Dani akasema:  
“Dani ni mwana simba,  
akiruka kutoka Bashani.”   
 23 Kuhusu Naftali akasema:  
“Naftali amejaa tele upendeleo wa Mwenyezi Mungu,  
naye amejaa baraka yake;  
atarithi magharibi na kusini.”   
 24 Kuhusu Asheri akasema:  
“Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri;  
yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake,  
yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.   
 25 Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba,  
nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.   
 26 “Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni,  
ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie,  
na juu ya mawingu katika utukufu wake.   
 27 Mungu wa milele ni kimbilio lako,  
na chini kuna mikono ya milele.  
Atamfukuza adui yako mbele yako,  
akisema, ‘Mwangamize yeye!’   
 28 Hivyo Israeli ataishi salama peke yake.  
Mzao wa Yakobo ni salama  
katika nchi ya nafaka na divai mpya,  
mahali mbingu hudondosha umande.   
 29 Ee Israeli, wewe umebarikiwa!  
Ni nani kama wewe,  
taifa lililookolewa na Mwenyezi Mungu?  
Yeye ni ngao yako na msaada wako,  
na upanga wako uliotukuka.  
Adui zako watatetemeka mbele yako,  
nawe utapakanyaga  
mahali pao pa juu.”