5
Kuenenda katika nuru
Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wanaopendwa, mkiishi maisha ya upendo, kama vile Al-Masihi alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.
Lakini uasherati usitajwe miongoni mwenu kamwe, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu wa Mungu. Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu. Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Mwasherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya (mtu kama huyo ni mwabudu sanamu) kamwe hataurithi ufalme wa Al-Masihi na wa Mungu. Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama hayo juu ya wale wasiomtii. Kwa hiyo, msishirikiane nao.
Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana Isa. Nendeni kama watoto wa nuru (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli), 10 nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana Isa. 11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. 12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini. 13 Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana, 14 kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana:
“Amka, wewe uliyelala,
ufufuke kutoka kwa wafu,
naye Al-Masihi atakuangazia.”
15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana Isa. 18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo mna upotovu, bali mjazwe Roho wa Mungu. 19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana Isa mioyoni mwenu, 20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba*Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi.
21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kutokana na kumcha Al-Masihi.
Mafundisho kuhusu wake na waume
22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama vile mnavyomtii Bwana Isa. 23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Al-Masihi alivyo kichwa cha jumuiya ya waumini, ambayo ni mwili wake, naye Al-Masihi ni Mwokozi wake. 24 Basi, kama vile jumuiya ya waumini wanavyomtii Al-Masihi, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.
25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Al-Masihi alivyoipenda jumuiya ya waumini na akajitoa kwa ajili yake, 26 kusudi aifanye takatifu, akiitakasa kwa kuiosha kwa maji katika neno lake, 27 apate kujiletea jumuiya tukufu isiyo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na isiyo na hatia. 28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. 29 Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Al-Masihi anavyoitunza jumuiya yake ya waumini. 30 Sisi tu viungo vya mwili wake. 31 “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 32 Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Al-Masihi na jumuiya ya waumini wake. 33 Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

*5:20 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.