6
Mafundisho kuhusu watoto na wazazi
Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana Isa, kwa kuwa hili ni jema. “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”
Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana Isa.
Mafundisho kuhusu watumwa na mabwana
Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa unyofu wa moyo, kama vile mnavyomtii Al-Masihi. Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Al-Masihi, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo. Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mngemtumikia, wala si wanadamu, mkijua kwamba Bwana Isa atampa kila mtu thawabu kwa lolote jema alilotenda, awe mtumwa au mtu huru.
Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi hiyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.
Silaha za Mwenyezi Mungu
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana Isa na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si dhidi ya mwili na damu, bali dhidi ya falme na mamlaka, dhidi ya wakuu wa ulimwengu huu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja, nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ivalishwe viatu vya utayari tunaopata katika Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho wa Mungu, ambao ni neno la Mungu, 18 mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.
19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.
 
Salamu za mwisho
21 Tikiko, aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana Isa, atawaambia kila kitu, ili pia mpate kujua hali yangu na kile ninachofanya. 22 Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali yetu, na awatie moyo.
 
23 Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Bwana Isa Al-Masihi.
 
24 Neema iwe na wote wanaompenda Bwana wetu Isa Al-Masihi kwa upendo wa dhati. Amen.