Kutoka
1
Waisraeli wagandamizwa
Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, kila mmoja na jamaa yake:
 
Reubeni, Simeoni, Lawi na Yuda;
Isakari, Zabuloni na Benyamini;
Dani na Naftali, Gadi na Asheri.
 
Wazao wote wa Yakobo walikuwa watu sabini; Yusufu alikuwa tayari yuko Misri.
 
Basi Yusufu na kaka zake wote na kizazi kile chote walikufa, lakini Waisraeli walikuwa wamezaana na kuongezeka sana, idadi yao ikawa kubwa mno, hadi wakaijaza nchi.
Kisha mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri. Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kuliko sisi. 10 Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana nasi, na kuondoka katika nchi hii.”
11 Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao. 12 Lakini walivyozidi kuteswa, ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi. Wamisri wakawaogopa Waisraeli, 13 kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili. 14 Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.
15 Mfalme wa Misri akawaita wakunga waliowazalisha Waebrania, ambao majina yao yalikuwa Shifra na Pua, akawaambia, 16 “Mtakapowazalisha wanawake Waebrania, chunguzeni wanapojifungua. Ikiwa ni mtoto wa kiume, muueni; lakini ikiwa ni msichana, mwacheni aishi.” 17 Lakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi. 18 Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?”
19 Wakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Waebrania ni tofauti na wanawake wa Misri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.”
20 Kwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi. 21 Kwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe.
22 Kisha Farao akatoa agizo hili kwa watu wake wote: “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania lazima atupwe katika Mto Naili, bali kila mtoto wa kike aachwe aishi.”