2
Kuzaliwa kwa Musa
Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi, naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu. Lakini alipoona hawezi kuendelea kumficha, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha kwenye matete kando ya ukingo wa Mto Naili. Dada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto.
Ndipo binti Farao akateremka kwenye Mto Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti Farao akaona kisafina kwenye matete, akamtuma mmoja wa wajakazi wake kukichukua. Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Waebrania.”
Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Waebrania akulelee huyu mtoto?”
Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto. Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea. 10 Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina Musa, akisema, “Nilimtoa kwenye maji.”
Musa akimbilia Midiani
11 Siku moja, Musa alipokuwa mtu mzima, alienda mahali walipokuwa ndugu zake, na akaona jinsi walivyokuwa wakifanyishwa kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmoja wa watu wake. 12 Musa akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha kwenye mchanga. 13 Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?”
14 Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.”
15 Farao aliposikia jambo hili, alijaribu kumuua Musa, lakini Musa akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima. 16 Kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza birika kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao. 17 Baadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Musa akainuka, akawasaidia kunywesha mifugo yao.
18 Wasichana hao waliporudi nyumbani, baba yao Reueli akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?”
19 Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikono ya wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.”
20 Akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.”
21 Musa akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Musa binti yake aliyeitwa Sipora amwoe. 22 Sipora alizaa mtoto wa kiume, naye Musa akamwita jina Gershomu, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
23 Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu. 24 Mungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka agano alilofanya na Ibrahimu pamoja na Isaka na Yakobo. 25 Kwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.