3
Musa na kichaka kilichowaka moto
Basi Musa alikuwa anachunga mifugo ya Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani. Musa akapeleka mifugo mbali nyuma ya jangwa, naye akafika Horebu, mlima wa Mungu. Huko malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea Musa katika mwali wa moto kutoka kichakani. Musa akaona kwamba ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. Ndipo Musa akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.”
Mwenyezi Mungu alipoona kuwa amegeuka ili aone, Mungu akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, “Musa! Musa!”
Naye Musa akajibu, “Mimi hapa.”
Mungu akamwambia, “Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” Kisha akamwambia, “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.” Musa aliposikia hayo, akafunika uso wake kwa sababu aliogopa kumtazama Mungu.
Mwenyezi Mungu akamwambia, “Hakika nimeona mateso ya watu wangu katika Misri. Nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, nami nimeguswa na mateso yao. Basi nimeshuka niwaokoe kutoka mkono wa Wamisri, niwatoe na kuwapandisha kutoka nchi hiyo, niwapeleke katika nchi nzuri na kubwa, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Sasa kilio cha Waisraeli kimenifikia, nami nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa. 10 Basi, sasa nenda. Ninakutuma kwa Farao ili kuwatoa watu wangu Waisraeli kutoka Misri.”
11 Lakini Musa akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata niende kwa Farao kuwatoa Waisraeli nchini Misri?”
12 Naye Mungu akasema, “Mimi nitakuwa pamoja nawe. Hii itakuwa ishara kwako kwamba ni Mimi nimekutuma: Utakapokuwa umewatoa watu Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.”
13 Musa akamwambia Mungu, “Ikiwa nitawaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa baba zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani?’ Nitawaambia nini?”
14 Mungu akamwambia Musa, “Mimi niko ambaye niko*au Nitakuwa kama Nitakavyokuwa; au, Mimi Ndiye. Hivyo ndivyo utakavyowaambia Waisraeli: ‘Mimi niko amenituma kwenu.’ ”
15 Vilevile Mungu akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo amenituma kwenu.’
“Hili ndilo Jina langu milele,
Jina ambalo mtanikumbuka kwalo
kizazi hadi kizazi.
16 “Nenda, ukawakusanye wazee wa Israeli, uwaambie, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, alinitokea akaniambia: Nimewatazama, nami nimeona mliyotendewa huku Misri. 17 Nami nimeahidi kuwapandisha kutoka kwenye mateso yenu katika nchi ya Misri, niwapeleke nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, nchi inayotiririka maziwa na asali.’
18 “Wazee wa Israeli watakusikiliza. Kisha wewe na wazee mtaenda kwa mfalme wa Misri na kumwambia, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania, ametutokea. Turuhusu twende safari ya siku tatu huko jangwani kutoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.’ 19 Lakini nafahamu kwamba mfalme wa Misri hatawaruhusu kwenda, hadi mkono wenye nguvu umlazimishe. 20 Kwa hiyo nitaunyoosha mkono wangu na kuwapiga Wamisri kwa maajabu yote nitakayofanya miongoni mwao. Baada ya hayo, atawaruhusu mwondoke.
21 “Nami nitawapa hawa watu upendeleo mbele ya Wamisri, kwa hiyo mtakapoondoka nchini hamtaondoka mikono mitupu. 22 Kila mwanamke Mwisraeli atamwomba jirani yake Mmisri na mwanamke yeyote anayeishi nyumbani mwake ampe vyombo vya fedha, dhahabu na mavazi, ambavyo mtawavika wana wenu wa kiume na wa kike. Hivyo mtawateka nyara Wamisri.”

*3:14 au Nitakuwa kama Nitakavyokuwa; au, Mimi Ndiye