11
Pigo la kumi: Kuuawa wazaliwa wa kwanza
1 Basi Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Nitaleta pigo moja zaidi kwa Farao na katika nchi ya Misri. Baada ya hilo, atawaacha mwondoke hapa na atakapofanya hivyo, atawafukuza mtoke kabisa. 2 Waambie watu wote kwamba kila mwanaume na kila mwanamke amwombe jirani yake vitu vya fedha na vya dhahabu.” 3 (Mwenyezi Mungu akawafanya Wamisri wawe na moyo wa ukarimu kwa Waisraeli, naye Musa mwenyewe akaheshimiwa sana na maafisa wa Farao na watu wote katika nchi ya Misri.)
4 Kwa hiyo Musa akasema, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Usiku wa manane, Mimi nitapita katika nchi yote ya Misri. 5 Kila mwanaume kifungua mimba katika Misri atakufa, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Farao, anayeketi kwenye kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mjakazi, anayesaga nafaka kwa jiwe, pamoja na kila mzaliwa wa kwanza wa mifugo. 6 Kutakuwa na kilio kikubwa katika nchi yote ya Misri, kilio ambacho hakijakuwa, wala kamwe hakitakuwa tena. 7 Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna hata mbwa atakayembwekea mwanadamu wala mnyama yeyote.’ Ndipo mtajua kuwa Mwenyezi Mungu huweka tofauti kati ya Misri na Israeli. 8 Maafisa hawa wako wote watanijia, wakisujudu mbele yangu, wakisema, ‘Ondoka, wewe pamoja na watu wako wote wanaokufuata!’ Baada ya haya nitaondoka.” Kisha Musa, akiwa amewaka hasira, akamwacha Farao.
9 Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Farao atakataa kukusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka katika nchi ya Misri.” 10 Musa na Haruni wakafanya maajabu haya yote mbele ya Farao, lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke katika nchi yake.