16
Mana na kware
Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani, jumuiya yote wakawanung’unikia Musa na Haruni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungekufa kwa mkono wa Mwenyezi Mungu huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tazama! Nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.”
Kwa hiyo Musa na Haruni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunung’unikie?” Kisha Musa akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Mwenyezi Mungu wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnung’uniki dhidi yetu, bali dhidi ya Mwenyezi Mungu.”
Kisha Musa akamwambia Haruni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake Mwenyezi Mungu, kwa maana amesikia manung’uniko yenu.’ ”
10 Haruni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa Mwenyezi Mungu ukitokeza katika wingu.
11 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 12 “Nimesikia manung’uniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
13 Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na utando wa umande kuzunguka kambi. 14 Umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya mchanga wa jangwa. 15 Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani.
Musa akawaambia, “Huu ndio mkate ambao Mwenyezi Mungu amewapa mle. 16 Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu ameamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi*yaani omeri moja, sawa na kilo mbili moja kwa kila mtu mliye naye katika hema lenu.’ ”
17 Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa; baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. 18 Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.
19 Kisha Musa akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote hadi asubuhi.”
20 Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Musa, wakahifadhi kiasi fulani hadi asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Musa akawakasirikia.
21 Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka. 22 Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Musa. 23 Musa akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Mwenyezi Mungu: ‘Kesho itakuwa Sabato ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke hadi asubuhi.’ ”
24 Kwa hiyo wakavihifadhi hadi asubuhi, kama Musa alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. 25 Musa akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. 26 Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwa chochote.”
27 Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote. 28 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu hadi lini? 29 Fahamuni kuwa Mwenyezi Mungu amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.” 30 Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.
31 Waisraeli wakaita ile mikate manamaana yake mkate kutoka mbinguni. Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama, na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali. 32 Musa akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza Mwenyezi Mungu: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ”
33 Kwa hiyo Musa akamwambia Haruni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za Mwenyezi Mungu ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.”
34 Kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa, hatimaye Haruni aliiweka ile mana ndani ya Sanduku la Ushuhuda ili aweze kuihifadhi. 35 Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani.
36 (Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efaEfa moja ni sawa na kilo 22..)

*16:16 yaani omeri moja, sawa na kilo mbili

16:31 maana yake mkate kutoka mbinguni

16:36 Efa moja ni sawa na kilo 22.