17
Maji kutoka mwamba
(Hesabu 20:1-13)
Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa. Kwa hiyo wakagombana na Musa wakisema, “Tupe maji ya kunywa.”
Musa akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu Mwenyezi Mungu?”
Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanung’unika dhidi ya Musa, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?”
Kisha Musa akamlilia Mwenyezi Mungu, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.”
Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Nenda mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, na uchukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende. Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Musa akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli. Naye akapaita mahali pale Masa*maana yake Kujaribu na Meribamaana yake Kugombana, kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Mwenyezi Mungu wakisema, “Je, Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi au la?”
Vita na Waamaleki
Waamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu. Musa akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”
10 Kwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Musa alivyomwagiza, nao Musa, Haruni na Huri wakapanda juu ya kilima. 11 Ikawa wakati wote Musa alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda. 12 Mikono ya Musa ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Haruni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Musa, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki thabiti hadi jua lilipozama. 13 Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.
14 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Andika mambo haya katika kitabu ili yakumbukwe, na uhakikishe kwamba Yoshua amesikia, kwa sababu nitafuta kabisa kumbukumbu la Amaleki chini ya mbingu.”
15 Musa akajenga madhabahu na kuiita Yehova Nisimaana yake Mwenyezi Mungu ni Bendera yangu. 16 Musa akasema, “Kwa maana mikono iliinuliwa dhidi ya kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu, sasa Mwenyezi Mungu atakuwa na vita dhidi ya Waamaleki kizazi hadi kizazi.”

*17:7 maana yake Kujaribu

17:7 maana yake Kugombana

17:15 maana yake Mwenyezi Mungu ni Bendera yangu