32
Ndama wa dhahabu
(Kumbukumbu 9:6-29)
1 Watu walipoona kuwa Musa amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimsonga Haruni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.”
2 Haruni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu, na binti zenu wamevaa, mkaniletee.” 3 Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Haruni. 4 Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akasubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”
5 Haruni alipoona hili, akajenga madhabahu mbele ya yule ndama na kutangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa Mwenyezi Mungu.” 6 Kwa hiyo siku iliyofuata watu wakaamka asubuhi na mapema na kutoa sadaka za kuteketeza na sadaka za amani. Baadaye watu wakaketi kula na kunywa, nao wakasimama, wakajizamisha katika sherehe.
7 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka. 8 Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kusubu yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ”
9 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu. 10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”
11 Lakini Musa akamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akasema, “Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu? 12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako. 13 Wakumbuke watumishi wako Ibrahimu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote niliyowaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ” 14 Kisha Mwenyezi Mungu akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.
15 Musa akageuka, akateremka kutoka mlimani akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma. 16 Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao.
17 Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Musa, “Kuna sauti ya vita kambini.”
18 Musa akajibu:
“Si sauti ya ushindi,
wala si sauti ya kushindwa;
ni sauti ya kuimba ninayosikia.”
19 Musa alipoikaribia kambi na kuona yule ndama na ile michezo, hasira yake ikawaka, akatupa vile vibao vilivyokuwa mikononi mwake, akavipasua vipande vipande pale chini ya mlima. 20 Kisha akamchukua yule ndama waliokuwa wamemtengeneza na kumchoma kwenye moto, kisha akamsaga kuwa unga, akanyunyiza kwenye maji na kuwafanya Waisraeli wanywe.
21 Musa akamwambia Haruni, “Watu hawa walikufanyia nini, hata ukawaongoza kufanya dhambi kubwa hivyo?”
22 Haruni akamwambia, “Usikasirike bwana wangu. Unajua jinsi watu hawa walivyo tayari kwa maovu. 23 Waliniambia, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza. Kwa kuwa huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.’ 24 Kwa hiyo nikawaambia, ‘Yeyote aliye na kito chochote cha dhahabu avue.’ Kisha wakanipa hiyo dhahabu, nami nikaitupa motoni, akatokea huyu ndama!”
25 Musa akaona kuwa watu wameasi, kwa kuwa Haruni alikuwa amewaacha waasi, na hivyo kuwa kichekesho kwa adui zao. 26 Kwa hiyo Musa akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa Mwenyezi Mungu, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.
27 Ndipo alipowaambia, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’ ” 28 Walawi wakafanya kama Musa alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao elfu tatu. 29 Kisha Musa akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.”
30 Siku iliyofuata Musa akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa Mwenyezi Mungu, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”
31 Hivyo Musa akarudi kwa Mwenyezi Mungu na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu. 32 Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kitabu ulichoandika.”
33 Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kitabu changu. 34 Sasa nenda, uongoze hao watu hadi mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”
35 Ndipo Mwenyezi Mungu akawapiga watu kwa ugonjwa wa tauni kwa sababu ya yale waliyoyafanya na ndama yule ambaye alitengenezwa na Haruni.