33
Amri ya kuondoka Sinai
1 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande hadi nchi niliyomwahidi Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’ 2 Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 3 Pandeni mwende katika nchi inayotiririka maziwa na asali. Lakini mimi sitaenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.”
4 Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yoyote. 5 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ” 6 Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima Horebu.
Hema la Kukutania
7 Basi Musa alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania”. Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa Mwenyezi Mungu, angeenda hadi Hema la Kukutania, nje ya kambi. 8 Wakati wowote Musa alipoenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Musa hadi aingie kwenye Hema. 9 Kila mara Musa alipoingia ndani ya Hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mwenyezi Mungu akizungumza na Musa. 10 Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la Hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake. 11 Mwenyezi Mungu angezungumza na Musa uso kwa uso, kama vile mtu anavyozungumza na rafiki yake. Kisha Musa angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka kwenye Hema.
Musa na utukufu wa Mwenyezi Mungu
12 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’ 13 Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.”
14 Mwenyezi Mungu akajibu, “Uso wangu utaenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.”
15 Kisha Musa akamwambia, “Kama Uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa. 16 Mtu yeyote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipoenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”
17 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nitakufanyia jambo lile uliloomba, kwa sababu ninapendezwa nawe, nami ninakujua kwa jina lako.”
18 Kisha Musa akasema, “Basi nioneshe utukufu wako.”
19 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, Mwenyezi Mungu, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.” 20 Lakini Mungu akasema, “Hutaweza kuuona uso wangu, kwa kuwa hakuna mtu yeyote awezaye kuniona akaishi.”
21 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Kuna mahali karibu nami ambapo unaweza kusimama juu ya mwamba. 22 Utukufu wangu unapopita, nitakuweka gengeni kwenye mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hadi nitakapokuwa nimepita. 23 Kisha nitaondoa mkono wangu nawe utaona mgongo wangu; lakini kamwe uso wangu hautaonekana.”