39
Mavazi ya Kikuhani
(Kutoka 28:1-14)
1 Kutokana na nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu akatengeneza mavazi yaliyofumwa kwa ajili ya kuhudumu katika mahali patakatifu. Pia akamshonea Haruni mavazi matakatifu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
Kizibau
2 Akatengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kitani iliyosokotwa vizuri. 3 Akafua vipande vyembamba vya dhahabu kwa nyundo na kutengeneza nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi, kazi ya fundi stadi. 4 Akatengeneza vipande vya mabegani vya kizibau, vilivyounganishwa kwenye pembe zake mbili kwa ajili ya kufungia. 5 Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi ulifanana nacho: ulikuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao ulitengenezwa kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
6 Akatengeneza vito vya shohamu vilivyowekwa katika vijalizo vya dhahabu, navyo vilichorwa na majina ya wana wa Israeli kama vile muhuri huchorwa. 7 Kisha akavifungia kwenye vipande vya mabega ya kizibau kuwa vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
Kifuko cha kifuani
(Kutoka 28:15-30)
8 Akatengeneza kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi. Akakitengeneza kama kile kizibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa. 9 Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja*Shibiri moja ni sawa na sentimita 22. na upana wa shibiri moja, nacho kilikunjwa mara mbili. 10 Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za vito vya thamani. Safu ya kwanza ilikuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi; 11 safu ya pili ilikuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi; 12 safu ya tatu ilikuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto; 13 katika safu ya nne ilikuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Vito hivyo vilitiwa kwenye vijalizo vya dhahabu. 14 Kulikuwa na vito kumi na viwili, kimoja kwa kila jina la wana wa Israeli; kila kimoja kilichorwa kama muhuri kwa jina mojawapo la makabila yale kumi na mawili.
15 Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani alitengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba. 16 Akatengeneza vijalizo viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, na kuzifungia pete hizo kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani. 17 Akafunga hiyo mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete katika pembe za hicho kifuko cha kifuani, 18 nazo zile ncha nyingine za mkufu akazifunga kwenye vile vijalizo viwili, na kuziunganisha na vile vipande vya mabega vya kile kizibau upande wa mbele. 19 Akatengeneza pete mbili za dhahabu na kuziunganisha kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibau. 20 Kisha akatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuziunganisha sehemu ya chini ya vipande vya mabega upande wa mbele wa kile kizibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kizibau. 21 Akafunga pete za hicho kifuko cha kifuani kwenye pete za kizibau kwa kamba ya buluu, wakiziunganisha na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwa kile kizibau, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
Mavazi mengine ya kikuhani
(Kutoka 28:31-43)
22 Akashona joho la kizibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, kazi ya mfumaji, 23 na lilikuwa na nafasi ya shingo katikati ya joho lile iliyofanana na ukosi, na utepe ulioshonwa kuizunguka nafasi hiyo ili isichanike. 24 Akatengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na ya kitani iliyosokotwa vizuri kuzunguka pindo la hilo joho. 25 Kisha akatengeneza vikengele vya dhahabu safi na kuviunganisha kuzunguka pindo hilo kati ya hayo makomamanga. 26 Hivyo vikengele na makomamanga vilipishana kuzunguka upindo wa joho ili livaliwe kwa kuhudumu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
27 Pia akamtengenezea Haruni na wanawe makoti ya kitani safi, kazi ya mfumaji, 28 na kilemba cha kitani safi, tepe za kichwani za kitani, na nguo za ndani za kitani iliyosokotwa vizuri. 29 Mshipi ulikuwa wa kitani iliyosokotwa vizuri ya rangi ya buluu, na zambarau, na nyekundu, kazi ya mtarizi, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
30 Kisha akatengeneza lile bamba, taji takatifu, kwa dhahabu safi na kuchora juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa:
Mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu.
31 Kisha wakalifunga kwa kamba ya rangi ya buluu ili kuliunganisha na kile kilemba, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
Musa akagua maskani ya Mungu
(Kutoka 35:10-19)
32 Kwa hiyo kazi yote ya maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania, ikakamilika. Waisraeli wakafanya kila kitu sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa. 33 Ndipo wakaleta maskani ya Mungu kwa Musa:
hema pamoja na vifaa vyake vyote, vibanio vyake, mihimili yake, mataruma yake, nguzo na vitako vyake;
34 kifuniko cha ngozi za kondoo dume kilichotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo†pengine ni mnyama mwenye ngozi laini aishiye kwenye milima yenye misitu, au pengine nguva au sili, na pazia la kufunikia;
35 Sanduku la Ushuhuda pamoja na mipiko yake na kiti cha rehema,
36 meza pamoja na vyombo vyake vyote, na mikate ya Wonesho;
37 kinara cha taa cha dhahabu safi, safu zake za taa pamoja na vifaa vyake vyote, pamoja na mafuta kwa ajili ya taa;
38 madhabahu ya dhahabu, mafuta ya upako, uvumba wenye harufu nzuri, na pazia la ingilio la hema;
39 madhabahu ya shaba, pamoja na wavu wa shaba, nguzo zake na vyombo vyake vyote,
sinia, na tako lake;
40 mapazia ya ua pamoja na nguzo na vitako vyake, pia na pazia la ingilio la ua;
kamba zake na vigingi vya hema kwa ajili ya ua;
vyombo vyote vilivyohitajiwa kwa ajili ya maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania;
41 na mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Haruni na mavazi ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.
42 Waisraeli walikuwa wamefanya kazi yote sawasawa na vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwagiza Musa. 43 Musa akakagua kazi na kuona kuwa walikuwa wameifanya sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameagiza. Kwa hiyo Musa akawabariki.